1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msaidizi mwingine wa Saddam anyongwa

Charles Mwebeya20 Machi 2007

Makamu wa rais wa utawala wa Saddam Hussein amenyongwa usiku wa kuamkia leo,ikiwa ni miaka minne kamili toka Marekani ilipoivamia Iraq kijeshi mnamo mwaka 2003.

https://p.dw.com/p/CB5B
Taha Yassin Ramadan enzi za utawala wa Saddam
Taha Yassin Ramadan enzi za utawala wa SaddamPicha: AP

Taha Yassin Ramadan makamu wa Rais wa utawala wa Marehemu Saddam Hussein amenyongwa usiku wa kuamkia leo akitumikia adhabu baadaya kuhusika na tuhuma za mauaji ya washia mnamo mwaka 1982.

Taarifa kutoka kwa ofisa mmoja mwandamizi kutoka ofisi ya waziri mkuu nchini Iraq, imesema adhabu hiyo imetekelezwa bila kasoro zozote .

Amesema Ramadan amenyongwa kwa tahadhari kubwa kuepuka makosa yaliyotokea kwa Saddam Hussein ambaye alidhihakiwa na mmoja wa wasaidizi wake Ibrahim AL Tikrit ambaye wakati wa kunyongwa kwake kichwa na kiwiliwili viliachana.

Ofisa huyo amesema watu walioshuhudia makamu huyo wa Rais wa zamani wa Iraq akinyongwa walikuwa ni maofisa kutoka ofisi ya waziri mkuu,mwendesha mashtaka, Jaji, maofisa kutoka wizara ya sheria pamoja na daktari.

Kwa mujibu wa mwanasheria wa Ramadan, kabla ya utekelezaji wa adhabu hiyo Ramadan alinukuliwa akisema haogopi kifo na kuwa atakufa kishujaa.

Kama ilivyokuwa kwa wasaidizi wengine wa Saddam Hussein, Taha Yassin Ramadan alikamatwa mnamo mwaka 2003 na wapiganaji wa kikurd ambao walimkabidhi wa majeshi ya Marekani na kufunguliwa kesi kuhusika na mauaji ya washia ya washia 148 katika kijijiji cha Dujail mnamo mwaka 1982.

Mtoto wa kiume wa Ramadan , Ahmed Ramadan akizungumza na kituo cha televisheni cha Al Jazeera mjini Sanaa –Yemen, amekiita kitendo cha kunyongwa kwa baba yake kama mauaji ya kisiasa.

Amesema mwili wa baba yake utazikwa katika mji wa Tikrit , karibu na mahala alipozikwa mtawala wa zamani wa nchi hiyo Saddam Hussein.

Ramadan amekuwa ni ofisa wa tatu kunyongwa toka Saddam Hussein aliponyongwa December 30, mwaka jana.

Wasaidizi wengine wa Saddam, Barzan Ibrahim AL Tikrit na Awad Ahmed Bandar walinyongwa January 15 mwaka huu kwa makosa ya mauaji na utesaji enzi za utawala wa Saddam Hussein.

Wakati huo huo Rais wa Marekani George Bush amesema bado ni mapema mno kuelezea tathmini ya majeshi yake yaliyoko Iraq kwa sasa.

Katika hotuba ya kuadhimisha miaka minne toka Marekani iivamie Iraq kijeshi mwaka 2003, amesema itachukua miezi kadhaa kupima matokeo ya ufanisi wa majeshi ya Marekani nchini Iraq.

Bush , amesema itakuwa ni maangimzi makubwa endapo vikosi vya ulinzi vya Marekani vitaondolewa nchini Iraq kabla ya muda uliopangwa.

Majeshi ya Marekani yanatakiwa kuhakikisha ulinzi na usalama nchini Iraq hadi September Mosi mwakani , lakini kumekuwepo na shinikizo kubwa kutoka kwa Maseneta wengi ndani ya Bunge la Congress wanaomtaka Rais Bush kuyaondoa majeshi ya Marekani nchini humo.

Bunge la Marekani ambalo kwa hivi sasa lina maseneta wengi wa chama cha upinzani cha Demokrat , wiki hii linatarajia kupitia makadirio na matumizi ya mpango wa ulinzi wa Marekani nchini Iraq , ikiwamo hoja ya kutaka kuyarejesha majeshi ya Marekani kutoka Iraq.

Ufanisi wa jeshi la Marekani nchini Iraq umekutana na changamoto kadhaa vikiwemo vitendo vya ulipuaji mabomu vinavyofanywa na vikundi vinavyohasimiana vya madhehebu ya Sunni na Shia ambapo maisha ya watu wengi yamepotea .

Kwa upande wake Marekani nayo imekwisha poteza wanajeshi wake 3,200 toka ilipoingia Iraq kwa mabavu mnamo mwaka 2003.