1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpira na mtandao

Ramadhan Ali28 Juni 2007

Kabumbu siku hizi pia limeingia katika mtandao na kila mchezaji dimba maarufu na mwenye jina hakosi mtandao wake.

https://p.dw.com/p/CHbr
Kupitia kipanya kuangalia kandanda
Kupitia kipanya kuangalia kandandaPicha: DW

Zile enzi ambapo mastadi wa dimba au mpira maarufu ikitosha tu kutamba uwanjani na kuwafurahisha mashabiki wao zimepita.Katika enzi za leo za mtandao,mashabiki wengi wanasaka njia nyengine za kuwasiliana na mastadi wao ili kujua zaidi juu yao.Kwa mfano,wachezaji na hata klabu mashuhuri za dimba leo zina mtandao wao binafsi.

Endapo ukitaka kujua mtandao wa mchezaji Fulani mashuhuri wa Ujerumani-mfano Michael Ballack,nahodha wa Ujerumani au kipa wa taifa Jens Lehmann sawa na wachezaji wengine kila mmoja ana mtandao wake.

Michael Ballack anaeichezea Chelsea,Frings-Werder Bremen na mshambulizi wa timu ya Taifa Miroslav Klose anaehamia Bayern Munich msimu ujao kutoka Bremen,hawajishughulishi binafsi na mtandao wao bali wanawaachia mabingwa wa mtandao kuwatembeza na kushughulikia.

Hata kipa wa Hamburg, Frank Rost mtandao wake unasimamiwa na shirika maalumu.Anasema:

“Bila shaka umbo na yaliomo katika safu mbali mbali za mtandao huo, ni kazi inayofanywa na wengine ,kwani binafsi si mudu kazi hiyo.Pia sina hamu ya kukaa masaa kadhaa mbele ya mtambo wa komputa ili kutayarisha.Lakini, kiliomo ndani ya mtandao huo kinatokana na mimi na kinanihusu mimi.”

Asema kipa Rost. Yote mamoja iwapo mtu atafungua mtandao wa Frank Rost au wa Michael Ballack au wa mjapani Naohiro Takahara,yaliomo ndani yake takriban yalingana na hayaelezi mengi ya kusangaza.Kuna picha nyingi na maelezo juu ya maisha ya mchezaji .

Kuna pia kadi za saini ya mchezaji.Isitoshe,kurasa si mara nyingi huwa na mapya isipokua ni maelezo yaliokwisha chapishwa zamani.Wakati mwengine taarifa alizoandika mchezaji mwenyewe zimeshapita wiki kadhaa.Hata ukurasa wa kipa wa hamburg Frank Rost uko hivyo lakini haoni yeye ni vibaya:

“Mtu hahitaji kuandika kila siku, kwani naona ni doro kufanya hivyo.Mtu anabidi tu kuandika panapozuka jambo muhimu au panapotokea kitu kwengineko cha kuzungumzia au kutoa taarifa- ndivyo naona barabara.”

Kila kukicha hadi wachezaji 500 wa Bundesliga-Ligi ya Ujerumani wana mtandao wao binafsi-homepage.Na Frank Rost anaona hii ni barabara.

Anasema kwamba kila mchezaji ,kila binadamu ambae ni maarufu hadharani anastahiki kuwa na kitu kama hicho-mtandao wake kwavile unamurika sura yake.Kwani, mtandao unampa nafasi ya kuelezea mambo jinsi aonavyo.

Na hii ni vizuri kabisa-asema Frank Rost.

Rost anaeleza zaidi kwamba, mtu haifai kumuachia mtu wa tatu kumsemea bali ajieleze binafsi anavyohisi.

Shabiki mmoja wa Jens Lehmann kipa wa taifa wa Ujerumani na wa Arsenal,London, alipogundua kuwa kipenzi chake hakina mtandao wake maalumu, aliamua kumfungulia binafsi.Mtandao huu kinyume na ule wa wachezaji wenyewe walio maarufu umeonekana kila mara una mapya na hauna tofauti kubwa na ule uliotayarishwa na mabingwa wa kazi hizo za kuandaa mtandao.Kipa Lehmann hakuhitaji kumlipa chochote shabiki huyo.