1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Urusi utaepusha mashambulizi Syria?

Beate Hinrichs10 Septemba 2013

Rais wa Marekani Barack Obama ameashiria kuwa atachelewesha kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria, iwapo utawala wa Assad utasalimisha silaha zote za Kemikali kwa jumuiya ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/19eeL
Syrian Foreign Minister Walid Muallem (R) and and his Russian counterpart Sergei Lavrov (L) walk to a press conference on September 9, 2013 following a meeting in Moscow. Muallem visits Russia for talks with the top global ally of Syrian President Bashar al-Assad as expectations grow of military action against the regime. Russia has vehemently opposed US-led strikes against the Assad regime, warning it could destabilize the whole Middle East, and President Vladimir Putin has vowed to help Syria if it was hit. AFP PHOTO / YURI KADOBNOV (Photo credit should read YURI KADOBNOV/AFP/Getty Images)
Sergei Lawrow und Walid Muallem Treffen in MoskauPicha: AFP/Getty Images

Rais wa Marekani Barack Obama ameashiria kuwa atachelewesha kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria, iwapo utawala wa Assad utasalimisha silaha zote za Kemikali kwa jumuiya ya kimataifa.

Pendekezo hilo lilitolewa na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, baada ya mkutano wake na mwenzake wa Syria, Walid al-Muallem. Hatua hii imepokelewa kwa wasiwasi na waandishi wa habari nchini Marekani lakini imekaribishwa na mataifa kadhaa yakiwemo Iran, Ujerumani, na Ufaransa.

Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wakichunguzi sampuli zilizotolewa nchini Syria.
Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wakichunguzi sampuli zilizotolewa nchini Syria.Picha: picture-alliance/dpa

Maswali yasiyo na majibu
Christiane Amanpour ni moja wa watangazaji wenye uzoefu mkubwa katika kituo cha televisheni cha CNN, lakini hata yeye hana uhakika ni jinsi gani Marekani itatathmini pendekezo la kustukiza kutoka Moscow na siri iliyoko nyuma ya pendekezo hilo. "Ama ni tukio lenye uzito, au ni mbinu ya kuchelewesha," alisema mtangazaji huyo maarufu wa Marekani.

Wasiwasi pia ulionekana katika taarifa ya kwanza rasmi kutoka serikali ya Marekani. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Marie Harf alisema haikuwa utukizi kwamba serikali ya Urusi imeamua kuchukua hatua baada ya kitisho cha mashambulizi.

Muda mfupi baadaye mshauri wa masuala ya usalama wa Obama Tony Blinken naye alikutana na waandishi wa habari na kuelezea wasiwasi kama huo, japokuwa yeye alikuwa muwazi zaidi. "Bila shaka tungelikaribisha iwapo Assad atasalimisha silaha zake za kemikali katika namna inayothibitika ili tuweze kuzidhibiti na kuziharibu. Hilo ndilo lengo letu, ili asiweze kuzitumia tena," alisema Blinken.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry.Picha: Reuters

Waandishi wa habari wa Marekani sasa wamechanganyikiwa, na wanataka kujua iwapo rais Obama atausubirisha mpango wake wa kuishambulia Syria. Na wanajiuliza iwapo waziri wa mambo ya kigeni John Kerry alikuwa anataka kutoa nafasi kwa diplomasia pale alipopendekeza mjini London, kuwa Assad anaweza kuepusha shamabulizi kwa kusalimisha silaha zote za kemikali kwa jumuiya ya kimataifa kabla ya mwisho wa wiki hii. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni na mshauri wa masuala ya usalama wamekuwa wakikwepa maswali hayo kutoka kwa waandishi.

Lakini waziri wa zamani wa mambo ya kigeni Hillary Clinton alisema iwapo Syria itakubali kusalimisha silaha zake za kemikali, hiyo itakuwa hatua nzuri. Lakini akaongeza kuwa kwa vyoyote vile, hii isiwe mbinu ya kuchelewesha, kwa vile Urusi inahitaji juhudi za jamii ya kimataifa ili kuungwa mkono, na kuongeza kuwa; "Mjadala huu unaweza tu kufanyika katika muktadha wa kitisho halisi cha kijeshi kutoka Marekani."

Kansela Merkel anena
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel naye anauona mpango uliopendekezwa na Urusi kama nafasi ya kutatua mgogoro wa Syria kwa njia za kidiplomasia.Katika kipindi maalumu cha uchaguzi katika televisheni ya umma ARD, Merkel aliyaelezea mapendekezo ya waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov kuwa ni mazuri.

"Leo Urusi imekuja na mapenedekezo mazuri, na kama kweli ilikuwa inamaanisha ilichokisema, na si mbinu ya kuchelewesha muda, basi Ujerumani Inaunga mkono kuchukuliwa kwa njia hiyo. Ni muhimu kujaribu njia zote pasipo kutumia nguvu za kijeshi na katika hili, ni muhimu tusubiri ripoti ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa," alisema Kansela huyo akijibu suali aliloulizwa na watazamaji, huku akisisitiza kuwa Ujerumani kamwe haiwezi kushiriki operesheni yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.Picha: AFP/Getty Images

Iran, China zaunga mkono, lakini wapinzani walia
Kwa upande wake, Iran nayo imekaribisha mpango huo wa Urusi, ambapo msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Marzieh Afgham, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mpango huo lazima uhusishe pia kuharibu silaha za kemikali zilizoko mikononi mwa waasi. China nayo ilisema kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya kigeni kuwa inakaribisha na kuunga mkono mpango huo wa Urusi.

Ufaransa ambayo ni nchi pekee barani Ulaya iliyonyesha utayari wa kushiriki mashambulizi dhidi ya Syria licha ya upinzani kutoka washirka wake, ilisema shinikizo la kimataifa limesaidia kuhusu Syria. Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian, amesema kuwa hii ni fursa nzuri inayostahili kutumiwa vizuri, na kuongeza kuwa Syria inapaswa kutekeleza mpango huo bila kuzunguka.

Lakini muungano wa upinzani wa Syria umesema mpango huo ni mbinu tu ya kisiasa yenye lengo la kuchelewesha mashambulizi, na ambao utasababisha vifo zaidi vya raia na uharibu.

Mwandishi: Ganslmeier Martin/Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afp
Mhariri: Daniel Gakuba