1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia unapingwa

Lillian Urio1 Agosti 2005

Waziri Mkuu wa Somalia, Ali Mohamed Gedi, amekataa mpango mpya ulipendekezwa na Umoja wa Mataifa, wenye kulenga kuziunganisha pande zote zinazogombana katika nchi yake.

https://p.dw.com/p/CHfa

Waziri Mkuu Gedi alisema mpango huo, uliotangazwa wiki iliyopita na Francois Fall, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia, ni suluhisho ambalo serikali yake inalazimishwa kulikubali.

Akizungumza na shirika la habari la kifaransa, AFP, Bwana Gedi alisema haina maana kuleta suluhisho bila kujadiliana na serikali ya Somalia na hawatakubali kulazimishwa kupokea suluhisho hilo.

Aliongeza kwa kusema serikali yake ina mpango wake wenyewe na ina mikakati ya kusuluhisha migogoro katika nchi hiyo. Alikubali kuwa wanahitaji kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa, lakini bado ni nchi huru.

Ijumaa iliyopita Bwana Fall alitangaza mpango mpya wa Umoja wa Mataifa wa amani nchini Somalia. Nchi hiyo haijakuwa na serikali halali kwa kipindi cha miaka 14 na bado ina matatizo makubwa, ingawa tangu mwaka jana serikali ya mpito iliundwa.

Jumatatu Bwana Fall anatarajiwa kuuwasilisha mpango huo kwa Waziri Gedi na rais wa mpito Abdullahi Yusuf Ahmed, ambaye sasa hivi wako kwenye mji wa Jowhar.

Jowhar ndio mji ambao serikali hiyo ya mpito ina makazi yake, tangu warudi kutoka Kenya mwezi uliopita, lakini kuna majadiliano makali ya wapi serikali ya nchi hiyo iwe na makazi yake.

Rais Yusuf na Waziri Mkuu Gedi wanasema kwa ajili ya usalama wao ni bora serikali hiyo ibaki Jowhar, kilomita 90 Kaskazini mwa Mogadishu na mji wa Baidoa kilomita 50 Kusini-Magharibi mwa Mogadishu.

Lakini sasa hivi Boidoa iko chini ya utawala wa mbabe wa kivita ambaye anapinga utawala wa rais Yusuf. Viongozi wa waasi walio mjini Mogadishu, pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ya mpito, akiwemo spika wa bunge, Sharif Hassan Sheikh Aden, wanataka makazi ya serikali yawe mjini Mogadishu.

Mpango wa Bwana Fall unapendekeza Jowhar kuwa makao makuu ya serikali ya Somalia. Kuundwa kwa Baraza la Taifa la Usalama ni kwa ajili ya kusimamia mpango mpya wa makubaliano ya amani, kusalimisha silaha na kuundwa kwa vikosi vya polisi na jeshi.

Mpango huo pia unataka kuwepo na mkutano kati ya serikali, bunge na Jumuiya ya Kimataifa ili kuisaidia serikali kuimarisha nchi ya Somalia.

Baada ya kukutana na Rais Yusuf na Waziri Mkuu Gedi mjini Jowhar, Bwana Fall anatarajiwa kwenda Mogadishu na kuwasilisha mpango huo kwa spika wa bunge bwana Aden, ambaye amekataa kuacha kushinikiza serikali ihamie Mogadishu.

Pamoja na kwamba inaonekana Bwana Aden na wababe wa kivita wa Mogadishu watapinga pendekezo la Bwana Fall, la makao ya serikali, Waziri Mkuu Gedi amesema serikali yake ya mpito ina mipango yake yenyewe juu ya usalama na sera za utawala.

Amesema wataunda upya vikosi vyao vya usalama, kutoka nchini kote bila kujali ukabila. Aliongeza kwamba kutoelewana katika serikali yake ni jambo la kawaida, linalotokea duniani kote, haimaanishi kwamba kuna mgogoro ndani ya serikali yake.

Waziri Gedi alisema baraza lake la mawaziri lina mawaziri 45, na ni watatu tu ambao hawakubaliani na wanajaribu kumhujumu spika wa bunge na mawaziri wenyewe watatu. Aliongeza kuwa asilimia 90 ya wakazi wa Mogadishu wanaunga mkono serikali.