1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa mashambulio ya Al-Qaeda Ulaya wagunduliwa

29 Septemba 2010

unasemekana unafanana na mashambulio ya Mumbai.

https://p.dw.com/p/PQ14

Mashirika ya ujasusi barani Ulaya yanasema yamegundua mpango wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda la kutaka kufanya mashambulio nchini Uingereza,Ufaransa na Ujerumani.Ripoti ya kituo cha matangazo ya televisheni cha Uingereza Sky News, ilisema kundi la walioandaa njama hiyo, wanaharakati wenye makao yao nchini Pakistan linasemekana kuwa na mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda, na mashambulio hayo yangefanywa wakati mmoja katika mji London na miji mengine kadhaa nchini Ufaransa na Ujerumani.

Duru za usalama nchini Uingereza zimekataa kusema lolote juu ya ripoti hiyo.Mhariri wa masuala ya kigeni wa kituo hicho cha televisheni Tim Marshall alisema kuongezeka kwa amashambulio nchini Pakistan mnamo wiki za hivi karibuni, kunahusiana na majaribio ya nchi za magharibi kuukandamiza mpango huo ambao, ulikuwa katika hatua za mwanzo mwanzo za maandalizi.

Kituo cha Sky News kimesema mashambulio hayo yangekuwa sawa na yale yaliofanywa na wanaharakati wa kipakistan ,katika hujuma ya ghafla mjini Mumbai-India 2008, pale watu waliokuwa na silaha nzito waliposhambulia sehemu kadhaa za mji huo ikiwemo hoteli maarufu ya Taj Mahal na stesheni kuu ya reli ya Mumbai.

Itakumbukwa mnamo mwezi Januari Uingereza ilitoa taarifa ikisema kiwango cha kitisho cha ugaidi wa kimataifa ni kikubwa zaidi.

Mkuu wa idara ya usalama ya Uingereza M15, Jonathan Evans alisema mnamo tarehe 16 mwezi huu wa Septemba, kwamba bado kunakitisho cha shambulio la gesi ya sumu.

Jana mjini Paris mnara maarufu wa Eiffel na maeneo yanayoizunguka bustani ya Champ de Mars yalizingirwa na polisi na kuwataka watu watawanyike, baada ya kupigwa simu na mtu asiyejulikana akisema kuna bomu lililotegwa, likiwa tukio la nne mjini Paris katika kipindi cha wiki kadhaa. Polisi walilipekua eneo hilo, lakini ikaonekana ni salama.

Tarehe 20 mwezi huu, Waziri wa ndani wa Ufaransa Brice Hortefeux alionya kuwa Uafaransa inakabiliwa na kitisho cha kweli cha ugaidi, kutokana na kundi la Al Qaeda katika Afrika kaskazini, kukiwa na wasi wasi wa mashambulio ya wafuasi wake ndani ya mipaka ya Ufaransa yenyewe. Kundi hilo linaloendesha harakati zake katika eneo la jangwani la nchi za Sahel,lingali likiwashikilia mateka Wafaransa watano mtoto mmoja na raia mmoja wa Madagascar baada ya kuwakamata hivi karibuni nchini Niger.

Kwa upande mwengine inachoonekana kuwa ni kuimarishwa kwa hujuma za ndege za kijeshi za Marekani dhidi ya wanaharakati wenye mafungamano na Al-Qaeda nchini Pakistan ,maafisa wa Marekani wanasema huenda kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa wanaharakati hao ameuawa. Sheikh Fateh al-Masri ambaye anasemekana aliteuliwa kuwa mkuu wa Al-Qaeda nchini Afghanistan na Pakistan, baada ya kuuwawa mtangulizi wake Mustafa al-Yazid mwezi Mei mwaka huu, alikufa katika shambulio hilo la karibuni kwenye eneo la mpaka wa nchi hizo mbili la Waziristan kaskazini.

Ama kuhusu kugunduliwa kwa mpango huo wa mashambulio katika miji kadhaa ya Ulaya, maafiasa wa Marekani wamekataa kufafanua hasa ni maeneo gani ya Ulaya ambayo yangeshambuliwa na wanaharakati hao, lakini wamekiri kuwa hujuma dhidi ya ngombe za wanaharakati hao nchini Pakistan zilikusudiwa kuivunja mitandao iliokuwa ikiandaa mashambulizi hayo.

Mwandishi:Mohammed Abdul-Rahman/AFP

Mhariri:Josephat Charo