1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa kichocheo cha uchumi wa Ujerumani waidhinishwa na bunge.

Sekione Kitojo20 Februari 2009

Bunge la wawakilishi wa majimbo nchini Ujerumani limeidhinisha mpango wenye thamani ya Euro bilioni 50 wa kichocheo cha uchumi.

https://p.dw.com/p/GyAV
Waziri wa fedha wa Ujerumani Peer Steinbrück (SPD) akizungumza siku ya Ijumaa katika bunge la wawakilishi wa majimbo , Bundesrat kabla ya kupitishwa kwa mpango mkubwa kabisa wa kichocheo cha uchumi katika historia ya Ujerumani.Picha: picture-alliance/ dpa


Bunge la Ujerumani limeidhinisha leo Ijumaa mpango mkubwa kabisa wa kichocheo cha uchumi katika historia ya nchi hiyo baada ya vita vikuu vya pili vya dunia, wenye lengo la kuuondoa uchumi mkubwa kabisa wa bara la Ulaya kutoka katika kuporomoka.


Hatua hiyo inaondoa kikwazo cha mwisho baada ya bunge la wawakilishi wa majimbo , Bundesrat, linalowakilisha majimbo 16 ya Ujerumani, kuidhinisha mpango huo. Serikali ya mseto inayoongozwa na kansela Angela Markel iliweka pamoja mpango huo wenye thamani ya Euro bilioni 50 mwezi uliopita baada ya juhudi zake za kwanza za mpango wa Euro bilioni 31 mwaka jana kukosolewa hapa nchini na nje ya nchi hiyo kwa kuwa ni mdogo mno.

Hatua hizo mpya pia zinajumuisha dhamana ya mikopo yenye thamani ya Euro bilioni 100, lakini kiasi hicho kinaripotiwa kuwa huenda kikapungua kutokana na msingi wa maombi ya mwanzo tu, limeandika gazeti la masuala ya biashara la Handelsblatt likinukuu duru kutoka wizara ya uchumi.

Iwapo tutaidhinisha maombi yote ambayo yamewasilishwa nje ya utaratibu, Euro bilioni 100 hazitatosha, zimesema duru kuliambia gazeti hilo.

Hatu hizo mbali mbali ni mpango mkubwa kabisa wa Ujerumani tangu baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Mpango huo unajumuisha ongezeko kubwa la matumizi katika ujenzi wa miundo mbinu pamoja na punguzo kubwa la kodi na mchango wa kugharimia huduma za jamii.

Takwimu rasmi zilizotolewa mwezi huu zinaonyesha kuwa uchumi wa Ujerumani umepungua kwa asilimia 2.1 katika robo ya mwisho ya 2008, ikiwa ni kushuka kwa kiwango kikubwa tangu Ujerumani mbili , ya mashariki na magharibi kuungana mwaka 2008. Kansela Angela Merkel amesema kuwa mpango huo ni mchango wa Ujerumani katika kutatua matatizo ya kiuchumi duniani.

Kwa kuwa na mpango huu mkubwa wa kichocheo cha uchumi katika historia ya nchi yetu, tunaonyesha uwajibikaji wetu kimataifa. Huu ni mzozo wa kiuchumi wa dunia na tunaweza tu kwa pamoja kuutatua, na Ujerumani inatoa mchango wake huu.


Ujerumani, ikiwa ni nchi ya kwanza duniani kwa kuuza bidhaa nje, ikiathirika kutokana na kupungua kwa mahitaji ya bidhaa zake nchi za nje , pamoja na kushuka kwa matumizi ya walaji ndani ya Ujerumani , imeingia katika mporomoko wa uchumi katika robo ya tatu ya mwaka 2008 baada ya kupungua kwa ukuaji wa uchumi mfululizo kwa kipindi cha miezi mitatu.

Mpango huo wa kuchochea uchumi unailazimisha Ujerumani kuchukua kiwango kikubwa cha madeni na waziri wa fedha Peer Steinbrueck amekiri kuwa nchi yake itavuka kiwango cha sheria ya nakisi ya umoja wa Ulaya.

Mpango huo umeidhinishwa na bunge la Ujerumani Bundestag , Ijumaa iliyopita. Serikali ya kansela Angela Merkel imetabiri kuwa uchumi wa nchi hiyo utanywea kwa asilimia 2.25 katika mwaka huu 2009.



Sekione Kitojo/AFPE.