1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto wauwa watu 12 na kujeruhi zaidi ya 70 London

14 Juni 2017

Moto uliosababisha maafa wakati wa usiku kwenye jengo la ghorofa 24 mjini London umeuwa watu 12 na kujeruhi wengine 74, watu 20 wako mahtuti.

https://p.dw.com/p/2eiE2
UK Mindestens sechs Tote und dutzende Verletzte bei Hochhausbrand in London
Picha: Getty Images/AFP/A. Dennis

Moto uliosababisha maafa wakati wa usiku kwenye jengo la ghorofa 24 mjini London umeuwa watu 12 na kujeruhi wengine 74 ambapo mwanamke amemrusha mtoto mchanga kutoka juu dirishani lakini mwanaume aliko chini ameweza kumdaka na kunusuru maisha ya mtoto huyo.

Moto huo uliun'garisha usiku na moshi mzito mweusi ulikuwa ukitoka kwenye madirisha ya jengo hilo la Grenfell Tower lilioko kaskazini mwa Kensington ambapo zaidi ya wazima moto 200 walikuwa wakipambana nao kuuzima. Ukungu mzito wa moshi ulikuwa umetanda kwa maili kadhaa mbiguni baada ya alfajiri na kuonyesha jinsi jengo hilo lilivyoteketea na moto huo ukiwa bado unaendelea kuwaka ikiwa ni zaidi ya masaa 12.

Kamishna wa kikosi cha kuzima moto cha London Dany Cotton ameuelezea moto uliolikumba jengo hilo kuwa usio na kifani kabisa.

Cotton amesema "Wafanya kazi wa zima moto wanaendelea kufanya kazi bila ya kuchoka kuzima moto ambao bado unaendelea kuwaka  na kuzipekuwa nyumba za jengo hilo .Kama mtakakavyokuwa mnatambuwa huo ni moto ambao hauna kifani kabisa.Katika historia yangu ya miaka 29 katika kikosi cha kuzima moto cha London sikuwahi kamwe kuona moto wa aina hii na nimeona moto ya majengo mengi ya ghorofa.Bila ya shaka suala hili litafanyiwa uchunguzi mkubwa lakini kwa wakati huu hututaki kuzungumzia zaidi juu ya sababu ya moto huo au kuenea kwake.Hilo ni jambo litakaloangaliwa kwa makini na katika kipindi cha hivi karibuni kabisa."

Kamishna huyo amesema  ana hofu askari wa zima moto wanaweza kugunduwa wahanga zaidi wakiwa bado wako ndani ya jengo hilo.

Kwa mujibu wa mashahidi watu waliokuwa kwenye nyumba za jengo hilo waliozingirwa na moto huo na moshi walikuwa wakigonga madirisha na kupiga makelele ya kuomba msaada kwa watu waliokuwa chini wakiangalia.Mmoja wa wakaazi amesema kin'gora cha kutowa tahadhari ya moto hakikulia.

Idadi ya vifo yumkini kuongezeka

UK Mindestens sechs Tote und dutzende Verletzte bei Hochhausbrand in London
Askari wa kuzima moto.Picha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

Kamanda wa polisi Suart Cundy ametowa idadi ya vifo lakini ameongeza kusema idadi hiyo yumkini ikaongezeka wakati wa opereshemi ya kuwatafuta manusura itakayochukuwa siku kadhaa.

Paul Woodrow mkuu wa operesheni za Magari ya kuwahudumia wagonjwa amesema watu 20 miongoni mwa waliojeruhiwa wako mahtuti.

Kwa mujibu wa shahidi mmoja mwanamkemke mmoja alimdondosha mtoto mchanga kutoka ghorofa ya tisa au ya kumi kwa watu waliokuwa njiani hapo chini.Mwanaume aliharakisha kumdaka mtoto huyo baada ya mwanamke huyo kuashiria kutoka juu dirishani kwamba anamrusha mtoto huyo.

Shirika la kiraia la Grenfell Action Group lilioundwa kupinga mradi wa kuendeleza eneo la karibu na hapo limekuwa likionya kuhusu hatari ya jengo hilo la Genfell Tower tokea mwaka 2013.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri :Yusuf Saumu