1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto mkali wawaka katika mji wa Haifa nchini Israel

Zainab Aziz
25 Novemba 2016

Wazima moto wanaendelea kupambana kuuzima moto huo mkali kwa siku ya nne leo katika mji wa Haifa nchini Israel. Maelfu ya watu wameyakimbia makaazi yao.  

https://p.dw.com/p/2TEVF
ISRAEL HAIFA Brände
Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

Takriban watu elfu 60 wameyakimbia makaazi yao  wakati ambapo polisi na vikosi vya wazimamoto wanapelekwa kwa wingi katika mji wa Haifa ambako inahofiwa kwamba moto huo mkali unaweza kuendelea kutokana na hali ya ukame inayoandamana  na upepo.  Watu kadhaa wamelazwa hospitali kutokana na madhara ya kuvuta moshi lakini hakuna taarifa zinazoashiria kuwa kuna watu walio katika hali mahututi.  Mamia ya nyumba za watu ziliharibiwa katika mkasa huo, Israel hapo jana ililazimika kuwaita maafisa wa jeshi wa akiba kuja kuungana na polisi wa nchi hiyo pamoja na wazima moto.  Vile vile maafisa hao waliitumia ndege maalum ya kupambana na moto mchango uliotolewa na jamii ya kimataifa.

Msemaji wa jeshi la polisi nchini Israel Micky Rosenfeld amesema shughuli za kuwahamisha watu zilifanyika jana usiku katika mji mdogo ulio karibu na jiji la Jerusalem baada ya nyumba kadhaa katika mji huo kushika moto.  Hadi kufikia sasa watu 12 wamekamatwa na wanatuhumiwa kuhusika na moto huo.  Viongozi wa Israel wanahisi kwamba moto huo umeanzishwa kwa makusudi na vijana wa Kiarabu. 
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amelaumu vitendo vya uchochezi moingoni mwa Wapalestina kuwa ndio chanzo cha mashambulio hayo.  Moto huo ulianza siku tatu zilizopita katika eneo la jamii ya Neve Shalom karibu na mji wa Jerusalem eneo ambalo jamii za Kiarabu na Kiyahudi zinaishi pamoja.  Baadae moto ulizuka upande wa kaskazini katika eneo la Zichron Yaakov na kwengineko karibu na mji wa Jerusalem kabla ya moto mkubwa kuanza katika mji wa Haifa.  Nchi kadhaa zikiwemo Urusi, Ufaransa, Cyprus, Uturuki,Croatia,Ugiriki na Italia zimetuma misaada yao ya kupambana na moto huo.  katika hatua isiyo ya kawaida Wapalestina pia wamejiunga na wazima moto wa Israeli kusaidia kuuzima moto huo.  

Golanhöhen israelischer Ministerpräsident Benjamin Netanjahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Getty Images/AFP/S. Scheiner

Maafa haya ni mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 2010 wakati Israel ilikumbwa na moto mkubwa uliowahi kutokea katika historia, moto huo ulisababisha vifo vya watu 42 na wazima moto waliweza kuuzima baada ya siku nne pale ndege maalum ya kuzima moto ilipofika kutoka Marekani na kutokea wakati huo Israel imeimarisha vifaa na jeshi lake la kupambana na moto, imenunua ndege maalum za kuzima moto ambazo zina uwezo wa kumwaga maji mengi katika eneo husika.

Mwandishi:  Zainab Aziz/APE

Mhariri:Yusuf Saumu