1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOSCOW: Lugovoi adai Waingereza walimuua Letvinenko

31 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBwE

Raia wa Russia anayetakikana nchini Uingereza kwa mauaji ya aliyekuwa jasusi wa shirika la ujasusi la Urusi ya zamani, KGB, Alexander Litvinenko, amewalaumu maafisa wa kijasusi wa Uingereza kwa mauaji hayo.

Andrei Lugovoi amewaambia waandishi wa habari mjini Moscow kwamba shirika la Ujasusi la Uingereza lilikuwa limemwajiri Alexander Litvinenko alikusanyie habari za rais wa Russia, Vladmir Putin, kibarua ambacho kilimchongea hadi ya kuuawa kwake.

Andrei Lugovoi amekanusha habari kwamba alihusika na mauaji hayo.

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza haijajibu moja kwa moja matamshi ya Lugovoi lakini imesema mauaji hayo ni suala la uhalifu wala si suala la kiusalama.

Juma lililopita serikali ya Uingereza iliitolea wito Russia kumrejesha Lugovoi ili ajibu mashtaka ya mauaji ya Alexander Letvinenko.

Katiba ya Russia hairuhusu washukiwa raia wa nchi hiyo kurejeshwa katika mataifa ya kigeni.

Alexander Letvinenko alifariki dunia mjini London mwaka uliopita kutokana na miale ya sumu.