1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco yapiga marufuku utengenezaji, uuzaji wa burqa

Mohammed Khelef
11 Januari 2017

Morocco imepiga marufuku utengenezaji na uuzaji wa vazi la burqa kwa kile kinachotajwa kuwa ni sababu za kiusalama katika taifa hilo la Kiarabu lenye Waislamu wengi kaskazini mwa Afrika.

https://p.dw.com/p/2VcS9
Symbolbild Frauentag
Picha: picture-alliance/dpa/Arshad Arbab

Shirika la habari la Le360 limemnukuu afisa wa ngazi za juu wa wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo, akisema hatua hiyo ni muhimu kwa amani na utulivu wa taifa hilo la Kiarabu kaskazini mwa Afrika. 

"Tumechukuwa hatua ya kupiga marufuku moja kwa moja uingizaji, utengenezaji na uuzaji wa vazi hili kwenye miji yote mikubwa na midogo ya Ufalme wa Morocco," alisema afisa huyo.

Taarifa hiyo inasema hatua hii imechochewa na wasiwasi wa ukosefu wa usalama, "kwani majambazi wamekuwa wakitumia vazi hili mara kwa mara kufanya uhalifu wao."

Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi ya serikali kuhusu amri hiyo ambayo inatazamiwa kuanza kutekelezwa rasmi wiki hii.

Wanawake wengi nchini Morocco, ambayo kiongozi wake, Mfalme Mohammed VI anapendelea Uislamu wa msimamo wa wastani, huvaa zaidi hijabu za kawaida kufunika kichwa tu kuliko burqa linalofunika mwili mzima.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo