1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moon amuonya jirani yake Korea Kaskazini

Sylvia Mwehozi
17 Mei 2017

Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In ameonya kwamba kuna "uwezekano mkubwa" wa kutokea mapigano ya kijeshi mpakani mwake na Korea Kaskazini wakati mvutano kuhusu matarajio ya Pyongyang kuhusu nyuklia ukiongezeka. 

https://p.dw.com/p/2d7kr
Südkorea Vereidigung Präsident Moon Jae-in
Picha: Getty Images/Chung Sung-Jun

Moon aliyeapishwa wiki iliyopita ameonya kwamba mpango wa Korea kaskazini wa nyuklia na maroketi  umekuwa "ukishika kasi", siku chache baada ya Pyongyang ilipoanzisha kile kinachonekana kuwa kombora la masafa marefu .

"Jeshi letu limedumisha utayari wa kijeshi ambao hautaruhusu uchokozi wa aina yoyote na tunayo dhamira na uwezo pindi ukihitajika mara moja na kuadhibu kwa nguvu, hata kama adui zetu wataleta chokochoko za silaha. Kama rais, nitaendeleza zaidi uwezo huo," alisema rais huyo.

Mvutano baina ya Washington na Pyongyang  umezidi kushika kasi katika wiki za hivi karibuni kutokana na utawala wa Trump kusema kwamba hatua za kijeshi zilikuwa ni njia mbadala inayozingatiwa na Korea kaskazini yenyewe ikitishia kulipiza kisasi kikubwa.

Rais Moon ambaye ana siasa za mrengo wa kushoto anapendelea ushiriki wa Korea kaskazini katika meza ya majadiliano lakini baada ya uzinduzi wa kombora siku ya Jumapili, kiongozi huyo amesema mazungumzo yatawezekana "ikiwa Pyongyang itabadili tabia yake".

Nordkorea Kim Jong-un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-unPicha: Reuters/KCNA

Korea kaskazini yenyewe ilidai kwamba roketi hilo linao uwezo wa kubeba kichwa cha kombora ingawa yapo mashaka ikiwa nchi hiyo inaweza kujenga kichwa kidogo kinachoweza kutoshea katika kombora.

Nchi hizo mbili za Korea, kiuhalisia ni kama bado ziko vitani baada ya mgogoro wa mwaka 1950-53 ulivyomalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano badala ya mkataba wa amani, mara kadhaa mataifa hayo yamesuguana katika mipaka yake.

Mashambulizi ya mabomu ya Korea kaskazini mwaka 2010 katika mpaka wa kisiwa cha kusini cha Yeonpyeong yaliwaua watu wanne katika shambulizi la kwanza dhidi ya raia tangu kumalizike kwa vita, na hivyo kuzua hofu ya mgogoro wa muda mrefu.

Eneo la mpaka ambako vurugu zilitarajiwa kuanza katika bahari ya njano kulishuhudia nyambizi la Korea Kusini likizama na kuwaua watu 46. Seoul ilituhumu shambulizi la kombora la majini la Korea Kaskazini ambayo kwa hasira ilikanusha ushiriki wake.

Korea ya Kaskazini imefanya majaribio mawili ya atomiki na mengine kadhaa ya makombora katika jitihada zake za utengenezaji wa kombora lenye uwezo wa kubeba kichwa cha nyuklia katika ardhi ya Marekani.

Kuongezeka kwa kitisho cha Korea Kaskazini kulisababisha Seoul katika siku za hivi karibuni kupeleka mfumo mkubwa wa Marekani wa kupambana na makombora licha ya kupingwa kwa hasira na China ambayo inaona kwamba ni kitisho kwa uwezo wake wa kijeshi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Saumu Mwasimba