1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mohamed Farmajo rais mpya wa Somalia

Grace Kabogo
9 Februari 2017

Waziri Mkuu wa zamani wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo amechaguliwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo, huku akiahidi kupambana na rushwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

https://p.dw.com/p/2XDQj
Somalia | Mohamed Abdullahi Farmajo
Picha: REUTERS/F. Omar

Farmajo mwenye umri wa miaka 55 na mwenye uraia wa nchi mbili Somalia na Marekani amemshinda rais aliyemaliza muda wake madarakani, Hassan Sheikh Mohamud, ambaye amekiri kushindwa baada ya duru ya pili ya uchaguzi huo uliofanyika jana, akisema uchaguzi ni wa kihistoria na Somalia imeitumia vizuri njia yake ya demokrasia.

Akizungumza jana baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo, Farmajo anayetoka kwenye ukoo wa Darod amesema ushindi huo ni mwanzo wa kuwepo umoja katika taifa la Somalia. ''Ushindi huu ni wa wananchi wa Somalia, mwanzo wa demokrasia na mapambano dhidi ya rushwa na Al-Shabaab. Nafasi ya urais sio kazi rahisi na kuna majukumu mazito yaliyoko mbele yangu. Nalijua hilo, lakini nitahakikisha nafanya kazi ya kutimiza ndoto zenu,'' alisema Farmajo.

Somalia Präsidentschaftswahl
Wabunge wa Somalia wakisubiri kupiga kura Picha: Reuters/F. Omar

Farmajo alishindwa kupata wingi wa theluthi mbili ya kura, lakini alipata kura 184 dhidi ya Mohamud aliyepata kura 97, hatua iliyomfanya rais aliyeondoka madarakani kukubali kushindwa ili kuepuka kufanyika uchaguzi wa duru ya tatu. Rais mwingine wa zamani, Sharif Sheikh Ahmed alipata kura 46. Farmajo alihitaji kupata kura 219 ili kuepuka duru ya tatu.

Kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, maelfu ya raia wa Somalia walimiminika mitaani kushangilia ushindi huo, huku wanajeshi wakifyatua risasi hewani pia kushangilia. Aidha, katika kambi ya wakimbizi wa Somalia iliyoko nchini Kenya ya Dadaad, iliripuka kwa shangwe na furaha kutokana na ushindi wa Farmajo huku wakiimbia wimbo wa taifa wa Somalia.

UN: Uchaguzi uligubikwa na madai ya rushwa na udanganyifu

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric amesema mchakato mzima wa uchaguzi uligubikwa na madai ya kuwepo rushwa na udanganyifu, huku wengine wakithibitisha kuhusika na madai hayo.

Mkuu wa kikosi cha Umoja wa Afrika cha kulinda amani nchini Somalia, AMISOM, Francisco Caetano Madeira ameutaka uongozi mpya wa Somalia kuitumia miaka minne ijayo kuongeza juhudi katika kuleta maridhiano na umoja. 

Kenia Nairobi Botschafter Francisco Caetano Jose Madeira
Mkuu wa AMISOM, Francisco Caetano Madeira Picha: DW/A. Kiti

Rais mpya wa Somalia, baba mwenye watoto wanne anawawakilishi Wasomali wanaoishi maeneo mbalimbali duniani kutokana na nchi hiyo kugubikwa na machafuko, lakini hatimaye wameanza kurejea nchini mwao kwa ajili ya kulijenga upya taifa lao. Wengi wa waliokuwa wagombea wa urais nchini Somalia, wana uraia wa nchi mbili.

Farmajo aliyezaliwa katika mkoa wa Gedo alihamia Marekani ambako alisomea historia na siasa ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Buffalo kilichoko mjini New York. Kiongozi huyo mpya alikuwa waziri mkuu wa Somalia kwa miezi minane, kati ya mwaka 2010 na 2011.

Aliondolewa madarakani katika mpango wa kuunda serikali mpya na kuahirisha uchaguzi mwaka huo. Farmajo pia aligombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2012, ukiwa ni uchaguzi wa kwanza kufanyika ndani ya nchi ya Somalia tangu mwaka 1991, ulipoanguka utawala wa Mohamed Siad Barre.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP
Mhariri: Saumu Yusuf