MOGADISHU:Wakazi waukimbia mji mkuu | Habari za Ulimwengu | DW | 12.04.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

MOGADISHU:Wakazi waukimbia mji mkuu

Mamia ya jamii za Kisomali wanaripotiwa kuutoroka mji wa Mogadishu ikiwa ni siku moja baada ya mapigano mapya kuzuka kati ya majeshi ya Ethiopia na wapiganaji wa mahakama za kiislamu.Mapigano hayo yanakiuka makubaliano ya amani yaliyofikiwa juma moja lililopita baada ya mazungumzo na makamanda wa majeshi ya Ethiopia.

Kulingana na wakazi wa Mogadishu hali ni ya wasiwasi baada ya mapigano hayo kuzuka.Mapigano hayo yaliyodumu siku nne ndiyo mabaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 15.

Takriban watu alfu 1 wamepoteza maisha yao katika mapigano yaliyotokea katika kipindi cha mwisho wa mwezi Machi na mwanzo wa mwezi Aprili.Wengine wanaripotiwa kuyatoroka makazi yao na kukimbilia maeneo yaliyo salama nje ya mji wa Mogadishu.

Kukiwa na mapigano ya aina hii inachukua muda mrefu kuwafikia wakazi kwani barabara zimefungwa na baadhi yake zina wapiganaji wanaoshambulia na kupora wakazi.Mpaka sasa ndege mbili zimedenguliwa na moja kati yao imedondoka mjini kwahiyo haiwezekani kufika katika uwanja wa ndege

Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la UNHCR yapata watu laki moja 24 wametoroka mjini Mogadishu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Viongozi wa kitamaduni wa ukoo wa Hawiye ulio na ushawishi mkubwa wanalaumu serikali kwa kuchagiza ghasia hizo zilizokiuka makubaliano ya amani yaliyodumu wiki moja.Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo na makamanda wa jeshi la Ethiopia.

Mapigano makali yalizuka mwezi jana baada ya majeshi ya Ethiopia kuanzisha msako wa wanamgambo wanaolaumiwa kushambulia ngome za serikali na majeshi ya Ethiopia mjini Mogadishu.

Nchi ya Somalia imekuwa bila serikali iliyo na nguvu tangu kungolewa madarakani kwa Mohammed Siad Barre mwaka 91.

Kwa upande mwingine majeshi ya Uganda yanayolinda amani nchini humo chini ya mpango wa Umoja wa Afrika yanasambaza maji safi na huduma za matibabu kwa majeruhi.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com