1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU:Meya wa Mogadishu ashambuliwa, wawili wauawa

21 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CC0A

Watu wawili wameuawa baada ya wanamgambo wa kisomali kuushambulia kwa bomu msafara wa meya wa jiji la Mogadishu.

Meya huyo wa Mogadishu Mohamed Dherre amesema kuwa waliyouawa ni raia na kwamba walinzi wake walifanikiwa kumpiga risasi na kumuua mpiganaji mmoja aliyekuwa juu ya mti wakati shambulizi hilo lilipofanywa.

Amesema kuwa wapiganaji wa Muungano wa Mahakama za Kiislam wanahusika na shambulizi hilo.

Wakati huo huo Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa limetaka kuchukuliwa kwa hatua za kimataifa kuwaondoa maharamia wa Kisomali katika pwani ya Somalia.

Wito huo unafuatia kushindwa kwa jaribio la maharamia hao kutaka kuiteka meli ya shirika hilo,karibu na bandari ya Merka kusini mwa Somalia hapo siku ya jumamosi.

Katika taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo la Chakula la Umoja wa Mataifa WFP, Josette Sheeran amesema kuwa iwapo hatua za kuzuia hali hiyo hazitachukuliwa watalazimika kusitisha shughuli zao za kusambaza misaada katika eneo hilo na kwamba hata mashirika mengine ya kimisaada yatasitisha kazi zao.