1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Watu saba wauwawa kwenye mripuko wa bomu

16 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCIX

Watu saba wameuwawa leo kwenye mripuko wa bomu karibu na mjini Mogadishu nchini Somalia.

Walioshuhudia wanasema mwanamke mmoja amepoteza mkono wake katika mripuko huo ambao umeziharibu nyumba mbili za wakimbizi waliokimbilia mjini Mogadishu.

Hapo awali Umoja wa Mataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu yamelaani mauaji ya mwaharakati wa haki za binadamu nchini humo.

Isse Abdi Isse, aliyekuwa zamani meya wa mji wa Kismayu, alipigwa risasi juzi Jumatano na majambazi wawili alipokuwa akinywa chai karibu na hoteli alimokuwa akiishi mjini Mogadishu.

Isse alikuwa mwenyekiti na muasiai wa shirika la amani na maendeleo la Kasima lililo na makao yake makuu mjini Kismayu.

Eric Laroche, mratibu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, amesema Isse alikuwa msitari wa mbele kupigania haki za binadamu katika eneo hilo na kifo chake ni pigo kubwa kwa Wasomali wote ambao kwa sasa wanatafuta amani na maridhiano.

Aidha kiongozi huyo amesema makundi ya kijamii yanalengwa katika mashambulio kwa sababu ya kazi yanayofanya nchini Somalia.