1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MOGADISHU: Serikali ya Somalia yakataa usitishwajji wa mapigano

2 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCD4

Serikali ya Somalia imekata usitishwaji wa mapigano baina ya majeshi ya Ethiopia na wanamgambo wa kiislamu mjini Mogadishu.

Mamia ya wananajeshi wa Ethiopia waliingia mjini Mogadishu hii leo baada ya siku nne za mapigano makali yaliyosababishwa na operesheni ya jeshi la Ethiopia dhidi ya wanamgambo wa kiislamu na wapiganaji wa kimbari.

Wakaazi wa Mogadishu wanasema wanajeshi hao wameingia mjini humo kupitia barabara inayotokea mjini Baidoa makao makuu ya serikali ya mpito ya Somalia.

Majeshi ya Ethiopia yanashika doria katika kitongoji cha Ali Kamin karibu na uwanja mkubwa wa kandanda, ambako mapambano makali yamekuwa yakiendelea na ambako kumesikika milio ya risasi mapema leo.

Balozi wa Marekani nchini Kenya, Michael Ranneberger, amesema Marekani ina wasiwasi juu ya machafuko ya Somalia na akazitaka pande husika zirejee katika meza ya mazungumzo.

Shirika la wakimbizi la Umoja wa mataifa, UNHCR, limetangaza kwamba Wasomali elfu 47 wameukimbia mji wa Mogadishu katika siku kumi zilizopita.