1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mnyamar: Idadi ya waliofariki imepita watu 15,000

Mwakideu, Alex6 Mei 2008

Mnyanmar yashutumiwa kwamba ilijua kuhusu uwezekano wa kutokea kimbunga hicho lakini haikuwatahadharisha wananchi wake mapema

https://p.dw.com/p/DuOz
Wananchi walioachwa bila makao wanautazama mti ulioangushwa na kimbunga cha NargisPicha: picture-alliance / dpa

Idadi ya watu waliofariki katika kimbunga cha Nargis nchini Mnyamar imepita 15,000 huku kukiwa na hofu ya kuongezeka zaidi kwa idadi hiyo.


Wahudumu misaada wa kimataifa wanasema baadhi ya manusura wa kimbunga hicho wangali wanaishi bila chakula, makaazi na hata maji ya kunywa tangu kilipotokea siku nne zilizopita.


Kimbunga hicho kimetajwa kuwa moja wapo wa mikasa mikubwa kuwahi kutokea barani Asia.


Utawala wa kijeshi wa Mnyanmar nchi iliyokuwa inajulikana kama Burma unalaumiwa kwa jinsi unavyoshughulika na janga hilo.


Kimbunga cha Nargis kilizoa vijiji katika mto wa Irrawaddy delta usiku wa ijumaa na kuzua maafa makubwa katika nchi ambayo tayari inatajwa kuwa moja wapo wa maskini zaidi duniani.


Akiongea na shirika la habari la AFP kwa njia ya simu mshauri wa shirika la msaada la kikristo World Vision Kyi Minn amesema wahudumu wa shirika hilo wameingia hadi katika maeneo yaliyoathirika zaidi kwa kutumia elikopta na kushuhudia miili ya watu.


Minn amesema janga hilo huenda likaleta maafa makubwa zaidi ya Tsunami iliyotokea mwaka wa 2004 kwani hakuna vifaa vya kutosha na vile vile usafiri umekuwa wa shida kubwa.


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewahakikishia wananchi wa Mnyanmar kwamba shirika hilo litasaidia.


Ban alisema "Umoja wa Mataifa utafanya kila uwezalo kutoa huduma zote za kibinadamu kwasababu ya mawasiliano duni hatuna uhakika wa kiasi cha hasara iliyotokea na vile vile waathiriwa, lakini nimeshtuliwa sana na habari zinazonifikia kwamba waliofariki wameongezeka na kupita elfu kumi tayari"


Licha ya utawala wa kijeshi nchini humo kujitenga na nchi zingine duniani na kuzuia mashirika mengi ya misaada kufanya kazi nchini humo, mashirika hayo yamemiminika na misaada ya kila aina ikiwemo vyakula, maji ya kunywa, mavazi na hata makaazi.


Waziri wan chi za kigeni Nyan Win alinukuliwa na vyombo vya habari hapo jana akikubali kwamba nchi yake ambayo imeongozwa na utawala wa kijeshi kwa miaka 46 inahitaji msaada wa kimataifa kwa dharura .


Awali Bi Laura Bush mkewe Rais Bush alitoa wito kwa Miayanmar kukubali misaada hiyo.


Bi Laura alisema "Tutafanya kazi na shirika la Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine ya kimataifa yasiokuwa ya kiserikali ili kuwapelekea maji, vyombo vya usafi, chakula na makaazi ya mda. Na misaada mingine itakuja baadaye. Marekani iko tayari kutoa kikosi chake cha msaada kwa Burma, punde tu serikali ya Burma itakapokubali misaada hiyo. Serikali ya Burma inahitaji kukubali kikosi hicho mara moja, na pia misaada mingine ya kimataifa"


Bi Laura ameushutumu utawala wa kijeshi nchini humo akisema ulifahamu kuhusu uwezekano wa kutokea kwa kimbunga cha Nargis lakini haukuwatahadharisha wananchi wake mapema.


Idadi ya waliofariki nchini Mnyanmar imekuwa ikiongezeka kwa hesabu ya watu 10 au hata 30 wakati hasara kamili ya kimbunga cha Nargis kilichovuma kwa kasi ya kilomita 190 kwa saa ikiendelea kujulikana rasmi.


Gazeti New Light of Mnyanmar ambalo sawa na vyombo vingine vya habari linaongozwa na serikali limeripoti kwamba hesabu ya hivi karibuni ya watu waliofariki imepita watu 15,000. Elfu kumi kati yao wamefariki mjini Bogalay.


Huduma za simu na umeme hazijarudi katika mji mkuu wa Yangon. Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya watu wameachwa bila makao katika mji huo pekee na unahofia kwamba huenda kukazuka mkurupuko wa magonjwa iwapo wakaazi wake hawatapata maji safi ya kunywa na makaazi.


Mnyanmar imekuwa ikishutumiwa na jamii ya kimataifa kwasababu ya kumfungia jela kwa miaka mingi mwana-demokrasia Aung San Suu ambaye ni mshindi wa tuzo la amani la Nobel.


Hata hivyo televisheni ya kitaifa nchini humo imeripoti kwamba kura ya maoni iliyokuwa inatarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki inatarajiwa kurejesha demokrasia na itaendelea kote nchini humo isipokuwa katika miji 47 iliyoathirika na kimbuka hicho.