1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkwe wa Osama ashtakiwa Marekani

Tsuma Carolyne8 Machi 2013

Mkwe wa kiume wa Osama bin Laden anatarajiwa kufika mbele ya mahakama moja mjini New York Marekani leo Ijumaa kwa mashtaka ya kupanga njama ya kuwauwa Wamarekani.

https://p.dw.com/p/17tqv
Suleiman Abu Ghaith Mkwe wa Osama bin Laden akamatwa na Marekani
Suleiman Abu Ghaith Mkwe wa Osama bin Laden akamatwa na MarekaniPicha: Reuters

Sulemain Abu Ghaith ambaye ni mwanamgambo aliyeonekana katika mikanda ya video akiwakilisha mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda baada ya mashambulio Septemba mwaka 2001,alikamatwa nchini Uturuki wiki iliyopita na kusafirishwa hadi Marekani kushitakiwa.

Abu Ghaith aliyezaliwa Kuwait amekuwa msemaji wa mtandao huo wa kigaidi na alikuwa mshirika wa karibu sana wa baba mkwe wake,Osama. Amekuwa akisifia sana mashambulio ya kigaidi ya septemba 11 mwaka 2001 na kuonya kuwa kutakuwa na mashambulio hata zaidi.

Kesi ni ushindi kwa Marekani

Kesi dhidi yake ni ushindi mkubwa kisheria kwa utawala wa Rais Barrack Obama ambao umekuwa ukitafuta kwa muda mrefu kuwashtaki washukiwa wakuu wanaohusishwa na Al Qaeda badala ya kuwazuia tu katika kambi ya kijeshi ya Guantanamo Bay iliyoko Cuba. Kuwashtaki washukiwa wakuu wa kigaidi katika mahakama za Marekani ilikuwa mojawapo ya ahadi kuu alizotoa Rais Obama punde tu baada ya kuchukua madaraka mwaka 2009 akilenga kufunga kambi hiyo ya Guantanamo Bay.

Barack Obama Rais Wa Marekani
Barack Obama Rais Wa MarekaniPicha: Reuters

Tetesi za magaidi kushtakiwa Marekani

Hata hivyo upande wa Republican umekuwa ukipinga nia hiyo ya serikali ya Obama na kulitokea tetesi kali alipofikishwa Abu Ghaith nchini humo. Wana Republican wanapinga kuletwa kwa washukiwa wakuu wa kigaidi nchini humo kwa hofu kuwa huenda ikaleta hata madhara zaidi kiusalama kwa taifa hilo iwapo kesi zao zitasikizwa na kuamuliwa katika mahakama za kawaida badala ya zile za kijeshi.

Mkuu wa sheria wa Marekani Eric Holder hapo jana Alhamisi alitangaza kukamatwa kwa Abu Ghaith na kusema hakuna jambo lolote litakalozuia azma yao ya kuwashtaki na kuwahukumu maadui wa Marekani.

Holder alikubali shingo upande mwaka 2011 kumshtaki Khalid Sheikh Mohammed aliyekiri kuwa mmoja wa wanachama wakuu wa Al Qaeda katika mahakama ya kijeshi ya Guantanamo Bay badala ya kiraia kutokana na shinikizo la Republican.

Attorney General Eric Holder gestures during a news conference at the Justice Department in Washington, Wednesday, April 11, 2012. (Foto:Cliff Owen/AP/dapd)
Eric Holder Waziri wa ulinzi wa MarekaniPicha: AP

Wizara ya ulinzi imesema Abu Ghaith ndiye msemaji wa Al Qaeda na alikuwa akifanya kazi kwa ukaribu na kiongozi wa sasa wa kundi hilo Ayman al Zawahri tangu mwezi Mei mwaka 2001 na kwamba amekuwa akiwataka wafuasi wao kuapa kuwa waaminifu kwa Osama Bin Laden.

Kulingana na kundi la kutetea haki za binadamau la Human Rights Watch,tangu mwaka 2001, washukiwa 67 wa kigaidi kutoka mataifa ya kigeni wameshtakiwa katika mahakama za Marekani.

Mwandishi:Caro Robi/AP

Mhariri: Saumu Yusuf