1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkwamo wanyemelea Thailand baada ya uchaguzi

2 Februari 2014

Uchaguzi Thailand umemalizika kwa salama Jumapili(02.02.2014)lakini mzozo wake mgumu wa kisiasa bado warindima wakati serikali ikikabiliwa na mkwamo utakaodumu kwa miezi kadhaa,maadamano na changamoto ngumu za kisheria.

https://p.dw.com/p/1B1dM
Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra akipiga kura yake mjini Bangkok . (02.02.2014)
Waziri Mkuu wa Thailand Yingluck Shinawatra akipiga kura yake mjini Bangkok . (02.02.2014)Picha: PORNCHAI KITTIWONGSAKUL/AFP/Getty Images

Upigaji kura ulitibuliwa kwa zaidi ya asilimia 10 ya majimbo ya uchaguzi nchini kote, lakini hakuna ghasia kubwa zilizoripotiwa licha ya kuzuka kwa mapigano ya silaha kati ya wafuasi na wapinzani wa Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra anayepigwa vita ambayo yamewajeruhi watu saba katika mkesha wa siku ya uchaguzi.

Tume ya Uchaguzi ya Thailand imeahirisha kutangaza matokeo ya uchaguzi huo Jumapili ikimaanisha hakuna mabadiliko makubwa juu ya hali ilioko hivi sasa nchini humo.Yingluck ataendelea kuwa waziri mkuu wa mpito kwa wiki kadhaa na kuendelea kukabiliwa na maandamano dhidi ya serikali na uwezekano wa kuibuka kwa changamoto za kisheria kuubatilisha uchaguzi huo.

Hata kama matokeo yatajulikana sherehe za ushindi wa Yingluck yumkini zikawa za kimya kimya,viti vingi bungeni vitakuwa vitupu na atashindwa kupitishwa miswada yoyote ile ya kisheria na bajeti ambazo ni muhimu kufufuwa uchumi wa nchi hiyo ambao ni wa pili kwa ukubwa Asia ya Kusini mashariki.

Waandamanaji wanaopinga serikali wakikabiliana na wafuasi wa serikali katika zoezi la kupiga kura Bangkok. (02.02.2014).
Waandamanaji wanaopinga serikali wakikabiliana na wafuasi wa serikali katika zoezi la kupiga kura Bangkok. (02.02.2014).Picha: Picture-Alliance/dpa

Demokrasia yavurugwa

Waandamanaji wanaopinga serikali wanasema Thaksin Shinawatra waziri mkuu wa zamani wa Thailand ambaye ni kaka wa Yingluck amevuruga demokrasia dhaifu ya nchi hiyo kwa kuanzisha siasa za fedha na kutumia fedha za walipa kodi kwa ajili ya takrima za ruzuku,huduma rahisi za matibabu na mikopo rahisi ambayo imempatia utii wa mamilioni ya wapiga kura wa tabaka la wafanyakazi kaskazini na kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Ikiwa na uungaji mkono mkubwa wa tabaka la kati mjini Bangkok,ukoo wa kifalme,vigogo wa fedha wa zamani na hata jeshi waandamanaji wanataka kusitishwa demokrasia nchini humo na badala yake kuteuliwa "baraza la wananchi " kuzifanyia mageuzi siasa za nchi hiyo na kupunguza ushawishi wa Thaksin.

Duru mpya ya machafuko katika mzozo huo wa miezi minane iliibuka hapo mwezi wa Novemba na kuonyesha dhima kuu ya Thaksin katika mzozo huo ambapo anaonekana kuwa ni shujaa halikadhalika adui.

Mwananchi wa Thailand akipiga kura yake Bangkok. (02.02.2014)
Mwananchi wa Thailand akipiga kura yake Bangkok. (02.02.2014)Picha: CHRISTOPHE ARCHAMBAULT/AFP/Getty Images

Yingluck kwa kiasi kikubwa alikuwa akivumiliwa na wapinzani wa Thaksin lakini chama chake kilikadiria vibaya mahesabu yake wakati kilipojaribu kuanzisha msamaha wa jumla ambao ungelitanguwa hatia ya rushwa aliokutikana nayo Thaksin na kumuwezesha kurudi nyumbani kutoka Dubai anakoishi uhamishoni.

Tume ya Uchaguzi imesema upigaji kura ulivurugwa kwa asilimia 18 au 69 ya majimbo ya kupiga kura 375 nchini kote na hiyo kuathiri majimbo 18 kati ya 77 ambapo waandamanaji wamefanikiwa kuhujumu uchaguzi huo.

Chama tawala kushinda kwa urahisi

Kutokana na chama kikuu cha upinzani cha Demokratik kususia uchaguzi huo ,chama cha Yingluck cha Puea Thai kinatazamiwa kushinda uchaguzi huo kwa urahisi.

Waandamanaji dhidi ya serikali wakiwa mbele ya visanduku vya kupiga kura wakijaribu kuvuruga zoezi hilo mjini Bangkok.(02.02.2014).
Waandamanaji dhidi ya serikali wakiwa meble ya visanduku vya kupiga kura wakijaribu kuvuruga zoezi hilo mjini Bangkok.(02.02.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wake amesema wananchi wanaiamini demokraisia.

"Watu hawaogopi na leo wamejitokeza kupiga kura" amesema hayo Jarupong Ruangsuawan ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani. "Tumepigania vikali demokrasia nchini Thailand na tumethibitisha kwamba Wathailand wengi wanaamini katika mchakato wa demokrasia."

Wachambuzi wanasema hata kama Yingluck atashinda na kuunda serikali mpya upinzani dhidi yake utaendelea kuwa mkali na kuendelea kwa mkwamo ni jambo la uhakika. Yingluck amesema anataraji makundi kadhaa yatatafuta njia ya kuondokana na mkwamo huo.

Amewaambia waandishi wa habari " Uchaguzi ni sehemu ya mchakato wa demokrasia. Natumai pande zote zitasaidia kutatua kila tatizo la nchi. Kwa jumla leo ilikuwa ni ishara nzuri."

Wathai wengi wanaona historia ikijirudia wenyewe kufuatia mkondo wa chaguzi kadhaa,maandamano ya upinzani na jeshi au mahakama kuingilia kati jambo ambalo limeigawa nchi hiyo na kuwakasirisha wafuasi wa Thaksin wanaovalia "fulana nyekundu " ambao wameapa kumhami dada yake dhidi ya jaribio lolote lile la mapinduzi.

Jeshi la Thailand hadi sasa halikupendelea upande wowote ule lakini mahakama imekuwa ikishughulikia kesi nyingi katika miezi miwili iliopita zikilalamika dhidi ya Yingluck na chama chake jambo ambalo linaweza kupelekea kuvunjwa kwa chama hicho na kupigwa marufuku kwa muda mrefu kwa wanasiasa wake waandamizi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mhariri: Iddi Ismail Ssessanga