Mkuu wa shirika la wakimbizi duniani-UNHCR- azuru Kongo mashariki | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkuu wa shirika la wakimbizi duniani-UNHCR- azuru Kongo mashariki

Janga la kibinadamu halivumiliki

default

Mkuu wa shirika la umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, Antonio Guterres, asema hali ya wakimbizi mashariki mwa DR Congo ni janga la kiutu.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusiana na wakimbizi la -UNHCR- Antonio GUTERRES anakamilisha jumatatu ziara yake ya siku tano katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Katika ziara yake hii ameweza kutembelea maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo kujionea hali ya wakimbizi ilivyo huko.

Mkuu huyo wa tume ya wakimbizi,ametoa masikitiko yake kutokana na kile kinachoweza kuitwa janga la kiutu mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Eneo hilo limekumbwa na mateso pamoja na mapigano mabayo yanafikia mwezi sasa kati ya vikosi vya serikali vikipambana dhidi ya vile vya Generali muasi Laurent Nkunda.

Akiwa mjini Goma –mji mkuu wa mkoa wenye matatizo wa kaskazini –mashariki, mwa Congo, kamishna amewaambia wandishi habari kuwa Umoja wa Mataifa ukishirikiana na mashirika mengine utaimarisha msaada zaidi katika eneo la Kivu Kaskazini kwa minajili ya kuboresha maisha ya watu waishio katika kambi za wakimbizi ambao wameachwa bila ya makazi na mapigano hayo.

Aidha ameongeza kuwa amani ni nyenzo muhimu ya kukomesha janga hilo.

Inakadiriwa watu zaidi ya laki 8 wamekimbia makazi yao katika mkoa huo kutokana na ghasia za miaka kadhaa. Karibu nusu ya watu hao imekimbia miezi 12 tu iliopita.

Kauli ya kamishana Guterres, imekuja wakati maofisa kutoka Congo,Rwanda,Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine ya kimataifa wakikutana mjini Goma kwa lengo la kujadilia mzozo huo,ambao wachunguzi wanahofia ,sio tu unatishia kujikakamua kwa kwa Congo kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini pia kutishia amani ya kanda hiyo.

Na baada ya mkutano huo, afisa wa Umoja wa Mataifa, amesema kuwa wameamua kuunda kamati ya pamoja itakayo kuwa na makao ya ke makuu mjini Goma.Jukumu kuu la kamati hiyo ni kuhakikisha amani na ushwari katika eneo la maziwa makuu.Naibu katibu mkuu wa umoja wa Mataifa-Haile Menkerios- amewaambia wandishi habari kuwa manai ya eneo hilo hayawezi kufikiwa hadi pale makundi yenye silaha,yawe ya wakongo ama raia wa kigeni yawe yamenyimwa nafasi ya kufanya shughuli zake huko.Amesema kuwa kazi ya tume hiyo itakuwa kuhakisha jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pamoja an Rwanda zinatekeleza mkataba wa nairobi wa mwezi Novemba.

Katika makubaliano hayo utawala wa Kinshasa ,uliahidi kukabiliana na waasi wa Kihutu wa Rwanda ambao wamejificha Kongo.Kigali kwa upande wake ilisema haitayaunga mkono makundi yoyote ya uasi ya wakongo,likiwemo lile la Generali mtoro,Laurent Nkunda.Mwishoni mwa juma kikosi cha kulinda amani nchini Kongo cha MONUC, kimeripoti kuwa wapiganaji wa Laurent Nkunda, wamerudi nyuma kutoka milima inayouzunguka mji wa Sake. Kiongozi wao ametaka mazungumzo na serikali.

Mapigano katika eneo hilo pia yanavihusisha vikundi kama vile wanamgambo wa Mai-Mai na wa wahutu kutoka Rwanda ambao ni maadui wa Nkunda.

Guterres amelaani kuwahusisha watoto katika makundi ya wapiganaji na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa wengi wao hupelekwa katika mstari wa mbele wa mapigano.

Kamishna huyo ameweza kutembelea kambi kadhaa za watu waliokimbia makazi yao. Na ziara yake nchini Kongo inakamilishwa leo.

 • Tarehe 17.12.2007
 • Mwandishi Siraj Kalyango
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CcdS
 • Tarehe 17.12.2007
 • Mwandishi Siraj Kalyango
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CcdS

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com