1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa wapinzani nchini Kenya washindwa kufanyika.

Halima Nyanza4 Januari 2008

Mkutano ulioitishwa na upinzani leo nchini Kenya ulishindwa kupata wafuasi kutokana na kuendelea kuwepo kwa idadi kubwa ya wanajeshi na askari wa usalama katika mji mkuu Nairobi.

https://p.dw.com/p/CkRb
Ulinzi umeimarishwa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.Picha: AP

Kwa upande mwengine Wakati hali bado ni tete Ufaransa imetoa taarifa kali, ambayo haijawahi kutolewa na nchi ya kigeni hadi sasa, ikikosoa udanganyifu uliofanywa katika kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa Bernar Kushner ameeleza kuwa suala la uchaguzi kukumbana na udanganyifu na mizengwe wengi wanalijua hilo, na kutolea mfano pia nchi kama Marekani na Uingereza kujua hali hiyo na kwamba wao pia wanaijua nchi hiyo ilivyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alikosoa yaliyotokea katika uchaguzi anasema, ninamnukuu, ’inaelezwa kuwa mapigano hayo yanayotokea nchini Kenya, ni ya kikabila, jibu ndio, lakini ni hali ya kawaida katika nchi za Afrika, pamoja na hayo hivi ni vita vya kupigania demokrasia.

Naye Waziri Mdogo wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika Bibi Jendayi Frazer anatarajiwa kuwasili leo mjini Nairobi kukutana na Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, anayedai kuny’ang’anywa ushindi wake baada ya upigaji kuwa wa Desemba 27 uliofanyika katika nchi hiyo ambayo inaongoza kiuchumi Afrika Mashariki, huku Rais George W Bush wa Marekani akiunga mkono juhudi za kimataifa katika kumaliza ghasia hizo kwa kusema kwamba, kuna fursa ya kukutana pamoja ili kuweza kusuluhisha tatizo hilo.

Wakati ulinzi bado ukiwa umeimarishwa mjini Nairobi hasa katika eneo la Uhuru Park, ambako wapinzani walikuwa wakutane, viongozi wa wapinzani wao, walikuwa wakikutana katika ofisi kuu, huku wakipokea wanadiplomasia waliokuja kutafuta suluhu ya mgogoro huo unaoendelea. Waandamanaji kadhaa jana walionekana kujitokeza katika eneo hilo la Uhuru Park, lakini hata hivyo polisi waliweza kuwadhibiti na kuwatawanya.

Zaidi ya watu 300 wamearifiwa kuuawa katika ghasia zilizodumu kwa wiki moja, wengine kutokana na mapambano kati ya polisi na wapinzani na wengine ni kutoka na vurugu za kikakila zilizozuka kati ya Wakikuyu na Wajaluo, huku watu wengine laki moja wakiyakimbia makazi yao.

Katika Hatua nyingine Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement ODM Anyang Nyong’o amesema kuwa chama chao kinamtaka Rais Kibaki kuachia madaraka, na kufanyika tena kwa uchaguzi mpya.

Katibu Mkuu wa ODM Anyang Nyong’o amesema nchi inapaswa kuwa tayari kwa uchaguzi mpya wa Rais.

Wapinzani pia walipanga kukutana tena leo lakini hata hivyo mpaka mapema ya leo hakukuwa na dalili za mkutano licha ya kuonekana kwa vikundi vidogo vya watu waliokuwa wakisema wanaandaa mkutano.

Amesisitiza kuwa uchaguzi huo unapaswa kufanyika katika kipindi kisichozidi miezi mitatu.

Maafisa wa kutoka vyama vinavyopingana nchini humo wamekuwa wakilaumiana kutokana na mapigano hayo yaliyobeba sura ya kikabila, lakini hata hivyo jana Rais Kibaki alitangaza kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na ODM.

Wakenya wako katika hali ya kupigwa na bumbuazi kutokana na machafuko hayo yaliyolikumba taifa hilo, ambalo ni maarufu katika masuala ya utalii, na pia ni kitovu cha ofisi nyingi za umoja wa mataifa, wanadiplomasia na mashirika ya misaada.

Ghasia hizo nchini Kenya, mbali na kuleta maafa kwa jamii pia zimekuwa zikileta madhara kiuchumi, Benki ya dunia imearifu kuwa ghasia hizo zinaweza kuathiri ongezeko la uchumi wa nchi hiyo, pamoja na kuathiri nchi nyingine katika ukanda huo hususan katika masuala ya biashara na usafiri.

Athari za kiuchumi pia nchini Kenya zimesababisdha kuzorota kwa mzunguuko wa fedha kutokana na mapigano yaliyotokea ambayo yamesababisha biashara mbalimbali kufungwa, lakini hata hivyo leo imeelezwa kuwa biashara zimeanza tena taratibu.

Uganda, Rwanda na Burundi tayari zimekumbwa na athari za machafuko hayo ya kisiasa yanayotokea nchini Kenya kutoka na kukabiliwa na tatizo la uhaba wa mafuta kufuatia kukwama kwa usafirishwaji kutoka bandari ya Mombasa.