1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa wakuu wa Bara la Amerika kuanza leo

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP/DPA16 Aprili 2009

Kisiwa kidogo cha Trinidad and Tobago hii leo kinakuwa taifa la kwanza katika eneo la Carribean kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi za bara la Amerika.

https://p.dw.com/p/HYQC


Kuwa mwenyeji kwa mkutano mkubwa kama huo, ambapo Rais Barack Obama wa Marekani ataudhuria, ni fahari kwa taifa hilo, lakini kwa upande wa pili ni kazi kubwa na nzito kuweza kuhimili mahitaji ya kiitifaki na kisualama kwa wakuu hao.

Jumla ya viongozi wa nchi 34 za bara hilo la Amerika wanaudhuria mkutano huo wa tano wa kilele, ambao kutokana na chagizo la Marekani, Cuba haiudhurii.


Kwa taifa hilo Trinidad and Tobago lenye wakaazi wahamiaji millioni 1.3, mkutano huo wa siku tatu ni nafasi muhimu kujitangaza.


Katika mji mkuu wa taifa hilo Port of Spain maandalizi yote kwa ajili kuwapokea kiasi cha wageni elfu tano watakaodhuria mkutano huo unaanza leo, yamekamilika.


Majengo yamepakwa rangi na maua yamepandwa kila mahali, huku vituo vya polisi vikitapakaa kote mjini.


Waziri Mkuu wa kisiwa hicho cha Trinidad and Tobago, Patrick Manning amesema kuwa ni wakati kwa taifa hilo dogo kudhihirisha kuwa lina uwezo wa kuandaa tukio kubwa kama hilo.


Katika kuimarisha usalama, nguvu imeongezwa kwa kuwasili maafisa usalama na polisi kutoka Jamaica, Belize, Barbados na Surinam pamoja na wengine kutoka Marekani na Brazil kudhibiti usalama wa anga na bahari.


Hoteli kubwa ya kitalii ambayo itatumika kama ukumbi wa mkutano huo, inaonekana kama ngome ya kijeshi iliyoko ufukweni mwa bahari.


Mbele ya hoteli hiyo kuna meli mbili kubwa za abiria ambazo zitatumika kwa ajili ya wageni, baada ya hoteli zote mjini humo kujaa.


Kila kitu kiko katika hali inayostahiki, ili kupunguza uwezekano wa kuwepo kwa maandamano ya kupinga mkutano huo, kama ilivyofanyika mwaka 2005 nchini Argentina wakati wapinzani wa sera na siasa za Marekani walipoandamana kumpinga Rais wa Marekani wa wakati huo George Bush.


Lakini kwa mrithi wake, yaani Rais Barack Obama amekuwa akipata umaarufu mkubwa katika eneo hilo la Latin Amerika, kwahivyo inaonekana hakutakuwa na upinzani kama ule aliyoupata Rais Bush huko Argentina.


Obama pamoja na viongozi wengine wameweka mazingira yatakayowezesha suala la Cuba lisiteke ajenda za kikao hicho, ambapo kwa ujumla nchi za Latin Amerika zinataka kuona Cuba inarejeshwa katika umoja huo.


Mwanzoni mwa wiki hii utawala wa Rais Obama ulitangaza kuondoa baadhi ya vikwazo vya usafiri na kutuma fedha kwao kwa wacuba wenye uraia wa Marekani.


Lakini vikwazo vya kiuchumi ambavyo viliwekwa na Marekani dhidi ya kisiwa hicho miaka 47 iliyopita bado vinaendelea.


Mapema Rais Evo Morales wa Bolivia alisema kuwa yeye pamoja na viongozi wengine masuhuba wa Rais Hugo Chavez wa Venezuela watatumia mkutano huo wa leo kumchagiza Rais Obama kubadilisha sera za Marekani kuelekea Latin Amerika.


Viongozi hao hapo jana huko Venezuela walikuwa na mkutano wa kuweka mikakati ya pamoja kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele hii leo.


Rais Morales amesema kuwa Rais Obama ameonesha kuwa na nia ya kufanya kile alichikiita ukarabati kutokana na uharibifu uliyofanywa na viongozi wa zamani wa Marekani.


Utawala wa Rais Bush ulikuwa na uhusiano mbaya na kundi hilo la Latin Amerika kutokana na wengi wa viongozi wake kuwa na mwelekeo wa kisoshalisti.

Mwandishi.Aboubakary Liongo

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman