1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa waarabu waijadili Syria

Admin.WagnerD29 Machi 2012

Mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu umeanza Alhamisi katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, kujadili mpango wa kurejesha amani nchini Syria. Wakuu wa nchi wapatao 10 wanashiriki katika mkutano huo.

https://p.dw.com/p/14UKO
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yakutana Baghdad kujadili mpango wa amani wa Syria
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yakutana Baghdad kujadili mpango wa amani wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Mkutano huu wa siku moja na wa kwanza kufanyika mjini Baghdad kwa kipindi cha miaka 20, unafanyika kukiwa na ulinzi mkali huku viongozi wa nchi wanachama wakitofautiana juu ya namna ya kumaliza mgogoro wa Syria, licha ya wote kukubaliana na mpango wenye vipengele sita wa mjumbe maalum wa Jumuiya hiyo na Umoja wa Mataifa, Koffi Annan.

Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alikutana na viongozi hao na kujadiliana nao juu ya utekelezaji wa mpango huo ambao unaungwa mkono pia na Umoja wa Mataifa.

Nabil El-Arabi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
Nabil El-Arabi Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za KiarabuPicha: dapd

Syria, ambayo hata hivyo haikualikwa kwenye mkutano huo, ilikubaliana na mapendekezo ya Koffi Annan, lakini ikasema haitakubaliana na hatua zozote zitakazochukuliwa na mkutano huo na imeongeza kuwa itajadiliana na nchi moja moja wanachama wa jumuiya hiyo, jambo ambalo linazidi kutatiza utekelezaji wa mpango wa Annan.

Shinikizo kuitaka Syria itekeleze haraka mpango wa Annan

Katibu Mkuu Ban alipongeza hatua ya Syria kukubaliana na mapendekezo ya mjumbe huyo na kusema kuwa inaleta matumaini ya kufikia mwafaka na kumaliza umwagaji damu unaoendelea nchini humo, lakini akazidi kumsihi Rais Bashar al Assad kutekeleza mapendekezo hayo haraka iwezekanavyo.

Ali al-Dabbagh, msemaji wa Mpango wa Makisio nchini Iraq akizungumza juu ya mkutano huo ameelezea matumaini juu ya mkutano huo. ''Tunaunga mkono kabisa juhudi za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria na tunadhani mawazo haya yanayoletwa na Mkutano wa Baghdad yatasaidia katika utekelezaji wa mpango wa Koffi Annan''. Alisema al-Dabbagh.

Wakati mataifa ya Kiarabu yakipinga hatua zozote kutoka nje ya jumuiya yao kuingilia kati mgogoro wa Syria, dalili zinaonesha kuwa mataifa hayo yameachana na mpango wao wa awali wa kumtaka Rais Assad akae pembeni na kumpisha naibu wake kuandaa mazungumzo.

Rais wa Syria Bashar al Assad (Kulia), na mjumbe kwa ajili ya Syria, Kofi Annan
Rais wa Syria Bashar al Assad (Kulia), na mjumbe kwa ajili ya Syria, Kofi AnnanPicha: picture-alliance/dpa

Mataifa ya Kisunni kama vile Saudi Arabia na Qatar yalikuwa yakishinikiza kutengwa kwa Syria na ikiwezekana waasi wapewe silaha, lakini mataifa mengine kama Algeria na Iraq yamesema lazima wawe makini katika hatua wanazochukua, wakihofia kwamba kuangushwa kwa utawala wa Assad kunaweza kusababisha vurugu za kiitikadi.

Mpango wa Annan unapendekeza, miongoni mwa mambo mengine, kuondolewa kwa zana nzito za kivita katika makaazi ya watu, kuruhusu msaada wa kibinadamu, kuachia huru wafungwa na kuruhusu waandishi wa habari wafanye kazi yao bila vizuizi.

Vurugu zaendelea Syria

Lakini wakati viongozi hao wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wakiendelea na mazungumzo mjini Baghdad, majeshi ya Syria yameendela kufanya mashambulizi na leo hii yameripotiwa kuuteka mji wa Saraqeb ulioko kaskazini mwa Syria, kufuatia siku nne za mapigano ambayo yameua watu zaidi ya 60 tangu jumapili iliyopita.

Iraq, ambayo inaanza kujijenga upya baada ya miaka kadhaa ya vita, inatumai kutumia mkutano huu kama njia ya kuonesha kurejea kwake katika ulingo wa diplomasia na inatafuta maridhiano na nchi za Kisunni zinahofia ukaribu wake na Iran.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/RTRE/DPAE

Mhariri: Mohamed Khelef