Mkutano wa viongozi wa upinzani Somalia waanza Asmara,Eritrea | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa viongozi wa upinzani Somalia waanza Asmara,Eritrea

Viongozi wa upinzani nchini Somalia wameanza mkutano wao wa siku kumi katika mji mkuu wa Eritrea,Asmara. Baadhi ya viongozi wa upinzani ambao wamekuwa mafichoni kwa karibu mwaka mmoja, wamejitokeza katika mkutano huo ili kutafuta jinsi ya kuviunganisha vikosi vyao kukabiliana na vile vya serikali ya mpito ya somalia inayoungwa mkono na Ethiopia.

Sheikh Sharif Sheikh Ahmed mkuu wa baraza la waislamu nchini Somalia katika mkutano na wanahabari.

Sheikh Sharif Sheikh Ahmed mkuu wa baraza la waislamu nchini Somalia katika mkutano na wanahabari.

Mkutano huo unaohudhuriwa na karibu wajumbe 400 unawadia wiki moja baada ya kukamilika kwa mkutano mwingine mjini Mogadishu ulionuia kuzipatanisha mbari mbalimbali nchini humo,mkutano uliofadhiliwa na serikali ya mpito na jamii ya kimataifa.

Sheikh Hassan Aweys kiongozi wa mahakama za kiislamu zilizosimamia eneo kubwa nchini Somalia kabla ya kufukuzwa na majeshi ya serikali kwa usaidizi na vikosi vya Ethiopia anahudhuria mkutano huo. Hii mni mara yake ya kwanza kujitokeza hadharini baada ya kuwa mafichoni kwa karibu mmwaka mmoja. Sheikh Aweys ,kiongozi mwenye imani kali ya kiislamu na wanachama wengine wa mahakama za kiislamu wanatafutwa na marekani kwa madai ya kuwa na mafungamano na mtandao wa kundi la kigaidi la al-qaeda.

Ripoti ya umoja wa mataifa mwaka jana ilimshutumu Aweys mwenye umri wa miaka 72 kwa kuendesha kambi za kutoa mafunzo ya kijeshi na kupokea silaha kutoka Eritrea kwa nia ya kuikorofisha ethiopia. Vikosi vya Ethiopia vinaunga mkono serikali ya mpito na wachanganuzi wa maswala ya kisiasa wanasema kujitokeza hadharani kwa Aweys katika mkutano huo mjini Asmara kunanuia kuighadhabisha ethiopia.

Sheikh Sharif Sheikh Ahmed kiongozi wa ngazi ya juu wa kiislamu katika hotuba yake katika mkutano huo wa Asmara alisema wanachohitaji ni kuondoka mara moja kwa vikosi vya Ethiopia ambayo vimeendelea kukalia somalia kinyume cha sheria. Kila aliyezungumza katika mkutano huo alisema iwapo hakutapatikana sulusisho la haraka mapigano yanayoendelea nchini somalia huenda yakasambaa hadi katika mataifa jirani na kusababisha hali ya wasiwasi kote barani africa.

Marekani , Ufaransa,I srael na jumuiya ya ulaya imewatuma wakilishi wao katika mkutano huo. Katika muda wa miaka mitatu sasa serikali ya mpito ya somalia inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi imeshindwa kuleta amani nchini humo. Inawalumu viongozi wa mahakama za kiislamu na wale wa mbari mbalimbali kwa kuchochea mashambulizi yanayofanywa kila siku mjini Mogadishu.

Tangu kupinduliwa kwa serikali ya Mohammed Said Barre mwaka 1991, Somalia hajakuwa na serikali na juhudi za kuzipatanisha pande zinazozozana hazijafua dafu.

 • Tarehe 06.09.2007
 • Mwandishi Jane Nyingi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH8P
 • Tarehe 06.09.2007
 • Mwandishi Jane Nyingi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH8P

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com