1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya umemalizika

25 Juni 2011

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekamilisha mkutano mkuu wa siku mbili mjini Brussels, Ubelgiji kwa kutoa idhini kwa nchi ya Croatia kujiunga na umoja huo.

https://p.dw.com/p/11jI1
Rais wa baraza la Ulaya Herman Van Rompuy, kulia, na waziri mkuu wa Croatia, Jadranka KosorPicha: dapd

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema kuwa taifa hilo lililokuwa sehemu ya iliyokuwa Yugoslavia, linapaswa kukamilisha majadiliano ya uanachama, wiki ijayo. Uanachama huo umeidhinishwa, baada ya miaka sita ya matayarisho yaliokumbwa na mageuzi ya taratibu ya kidemokrasia katika nchi hiyo na kusita kwa Umoja huo kupanuka. Wanadiplomasia wanasema, Croatia inatarajiwa kuwa mwanachama wa 28 wa Umoja huo ifikapo Julai mwaka 2013. Kabla ya tangazo hilo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, alisema kuwa hakuna vizuizi vyovyote kwa Croatia kujiunga na Umoja wa Ulaya.

EU Kroatien EU-Gipfel hat den Weg für einen Kroatien Beitritt 2013 frei gemacht
Bendera za Croatia, na Umoja wa Ulaya zimeangikwa bungeni CroatiaPicha: dapd

Kutokana na ombi la Ufaransa, Uholanzi na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya, mfumo mkali wa ukaguzi unapaswa kuidhinishwa, ili kuhakikisha kuwa Croatia inafuatiliza mageuzi iliyoahidi kufanya katika mfumo wake wa sheria.

Hapo jana viongozi hao pia walimuidhinisha kiongozi mpya wa Benki Kuu ya Ulaya. Muitalia, Mario Draghi anachukua nafasi ya Mfaransa, Jean Claude Trichet, anayejiuzulu ifikapo mwezi Oktoba.

Uteuzi wa Draghi ulitarajiwa kutangazwa siku ya Alhamisi lakini ulicheleweshwa kwa siku moja baada ya Ufaransa kupinga, ikisema uteuzi wake ungemaanisha kuwa Ufaransa haitowakilishwa katika Bodi ya Benki hiyo kuu ya Ulaya. Ufaransa ilimuidhinisha Draghi, baada ya Muitalia mwingine, katika bodi hiyo, Lorenzo Bini Smaghi, hapo jana kukubali shingo upande, kujiuzulu mapema.

Wakati huo huo viongozi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kuwa nchi wanachama wa umoja huo, ziweze kuanzisha upya kwa muda ukaguzi wa mipakani katika kanda ya Schengen, iwapo patakuwepo sababu ya dharura kufanya hivyo.

EU-Gipfel in Brüssel
Rais wa halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel BarrosoPicha: dapd

Nchi kadhaa za Umoja huo wa Ulaya zimeeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko lisilo la kawaida la wakimbizi kutoka maeneo ya Balkan ya Magharibi, na wahamiaji wengi wanaoingia kutoka Afrika Kaskazini.

Katika taarifa yao, viongozi wa Umoja wa Ulaya wamesema, kuna haja ya kuanzisha mfumo utakaoziruhusu serikali kuchukuwa hatua haraka, katika hali zisizo za kawaida, bila ya kuhatarisha uhuru wa watu kusafiri. Eneo hilo la Schengen ambapo mtu anaweza kusafiri bila ya pasipoti, ni msingi mkuu wa sera ya mipaka wazi ya Ulaya na ya kujumuisha jamii mbalimbali.

Mwandishi: Maryam, Abdalla
Mhariri: Martin, Prema