1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa usalama mjini Munich

Oumilkher Hamidou9 Februari 2009

Siasa ya nje ya Marekani itakua ya aina nyengine kabisa anasema kamo wa rais Joe Biden

https://p.dw.com/p/GpxA
Makamo wa rais wa Marekani akihutubia mkutano wa usalama mjini MunichPicha: AP


Siasa ya nje ya Marekani na hasa ushirikiano pamoja na nchi za Ulaya itakua ya aina gani siku za mbele?Suala hilo limejibiwa kwa sehemu kwa hotuba ya makamo wa rais wa Marekani Joe Biden katika mkutano wa usalama mjini Munich na kupokelewa kwa moyo mkunjufu na wajumbe mkutanoni.



Siasa ya nje ya Marekani itapitiwa kwa dhati-amesema hayo bila ya kificho, makamo wa rais wa Marekani Joe Biden katika hotuba yake ya kwanza barani Ulaya.Kitakachobadilika katika utawala wa Barack Obama,sio tuu muongozo bali pia namna yenyewe ya kuendeleza siasa ya nje.



"Kwa niaba ya Barack Obama,ningependa kusema:Siasa ya nje ya Marekani itakua ya namna mpya."



Zimeshapita enzi za maamuzi ya upande mmoja ya Marekani,umepita wakati wa kutojua nini cha kusema maoni ya watu yanapotofautiana.Serikali ya Obama inapanga kusaka ufumbuzi wa matatizo,kupitia mazungumzo na kwa ushirikiano,anasema Joe Biden na kupigiwa makofi na washirika mkutanoni.



"Jumuia na mashirika ya kimataifa hayadhoofishi nguvu za Marekani,yanaimarisha usalama wetu,uchumi wetu na hadhi yetu.Kwa hivyo tutawajibika,tutasikiliza na tutasaidia.Marekani inaihitaji dunia na dunia inaihitaji Marekani".


Mtindo wa kushirikiano,anasema makamo wa rais wa Marekani,haumaanishi kwamba Marekani itaregeza kamba.Washington itasaka njia za kuzungumza na Iran lakini itaendelea kuishinikiza iachilie mbali mpango wake wa kinuklea.Marekani ingali inapendelea kutega mitambo ya kinga ya makombora katika Ulaya ya  Mashariki,lakini inataka kuzungumzia suala hilo pamoja na Urusi.Kwa jumla Marekani inataka kusawazisha ushirikiano wake na Urusi amesisitiza makamo wa rais wa Marekani Joe Biden.


Marekani inataka kufanya mengi zaidi,lakini pia inategemea mengi zaidi kutoka kwa washirika wake-anasema Joe Biden.Watu wa ulaya pia wanabidi wabebe sehemu yao ya mzigo-mfano nchini Afghanistan.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anasema haoni kama kuna maajabu ya kushangaza yatakayotokea:



"Sioni mie kama Ujerumani itatakiwa iwajibike kupita kiasi.Kinyume kabisa.Leo pia nimesikia jinsi maamuzi yetu yalivyosifiwa,naiwe linapohusika suala la kuzidisha juhudi za kiraia za ujenzi mpya au  linapohusika asuala la kuzidisha idadi ya wanajeshi na kufikia 4500."


Msaada,serikali ya Marekani inategemea katika suala la kupokelewa wafungwa wa kutoka kambi ya Guantanamo,amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Steinemeier.Makamo wa rais wa Marekani Joe Biden amesema kwa mara nyengine tena mjini Munich,kambi hiyo itafungwa na hakutokua tena na mateso.