1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Trump na Macron na wito wa kuvumiliana magazetini

Oumilkheir Hamidou
25 Aprili 2018

Mada mbili tu zimehanikiza magazetini : Mazungumzo kati ya rais wa Marekani Donald Trump na mgeni wake wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Washington, na hofu za kuibuka upya hisia za chuki dhidi ya wayahudi.

https://p.dw.com/p/2wcNv
USA Washington - Donald Trump trifft Emmanuel Macron
Picha: Reuters/K. Lamarque

Wahariri wengi wa magazeti ya Ujerumani wanakubaliana "mapokezi ya kifahari na madaha aliyoandaliwa rais wa Ufarana Emmanuel Macron hayakuweza kuficha tofauti kubwa zilizoko katika misimamo ya rais wa Marekani Donald Trump na mgeni wake Emmanuel Macron".Gazeti la "Heilbronner Stimme" linaandika: "Donald Trumpo anauangalia umoja madhubuti wa Ulaya kama kitisho kwake. Ili kuleta mtengano, makubaliano ya nafuu za kodi ziada kwa taifa moja moja, yanaweza kumsaidia. Mageuzi ya kiuchumi ya Emmanuel Macron yanahitaji kichocheo.

Lakini  mwenyewe rais wa Ufaransa anapigania Ulaya yenye nguvu na imara. Anapigania Ulaya ambayo miongoni mwa mengineyo itakuwa tayari kuwajibika zaidi katika siasa ya nje ya kimataifa. Na kwa namna hiyo Macron ana msimamo sawa na Merkel.Makubaliano ya mradi wa nyuklia wa Iran kwa mfano, Ufaransa, sawa na Ujerumani na Umoja wa Ulaya wanataka yaendelezwe. Mada hiyo itajadiliwa pia kansela Merkel atakapofika ziarani Ijumaa inayokuja mjini Washington. Mbinu stadi za Macron zimevunja kiburi cha Trump anaehisi hapewi umuhimu mkubwa na kansela Merkel.

Hofu za kuzidi hisia za chuki dhidi ya Wayahudi

 

Mjadala umepamba moto dhidi ya kitisho cha kuenea hisia za chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Mshikamano katika kupambana na hisia za chuki dhidi ya wayahudi ndio kauli mbiu.Mjadala kuhusu mashairi dhidi ya Wayahudi katika muziki wa Rap, kanda inayotisha ya video inayoonyesha shamabulio dhidi ya kijana aliyevaa kikofia cha wayahudi-Kippa" mjini Berlin, maadhimisho ya miaka 70 tangu kuundwa taifa la Israel-yote hayo yameshuhudiwa wiki iliyopita na kugubika ajenda ya kisiasa humu nchini.

Lakini kama kawaida, watu wanapokusanyika  neno mshikamano hutumika ndivyo sivyo na kwa namna hiyo kutishia kupoteza umuhimu wake. Hisia za chuki dhidi ya Wayahudi watu hawawezi kupambana nazo kwa siku moja tu.Hisia kama hizo haziko pekee vichwani mwa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wanazi mambo leo pamoja na wafuasi wa itikadi kali ya Kiislam bali zimeota mizizi vichwani mwa watu na kuchukua sura ya dhana mbaya zinazozidi kupata nguvu."

 

Hisia za chuki zisiachiwe Ujerumani

Gazeti la "Rhein Necker" linaandika:"Tunavaa Kippa. Na pengine tungebidi kuvivaa kwa wingi hadharani tangu zamani ili kuondowa hali ya kutoelewana. Kwamba nchini Ujerumani lawama dhidi ya Israel kama zinavyofanya serikali za nchi takriban zote zinaruhusiwa na halali, lakini lawama  hazimaanishi moja kwa moja upinzani, bali katika kadhia maalum, ni malumbano ya maana.

Tunavaa Kippa, tunavaa hijab.Tunavaa kwa wingi wetu msalaba.Yote hayo ni sehemu ya Ujerumani. Na huo kwa kweli ni ujumbe bayana wa kuvumiliana.Tumalizie kwa kukumbusha matamshi ya mmojawapo wa marais wa zamani wa ujerumani aliyesema"Hisia za chuki si sehemu hata kidogo ya Ujerumani."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga