1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa tabia nchi umeanza leo mjini Warsaw

Mohamed Dahman11 Novemba 2013

Wajumbe wa masuala ya mazingira kutoka nchi tajiri, zinazoinukia kiuchumi na visiwa vilioko hatarini kutoweka wanakutana Poland kwa wiki mbili kuweka misingi ya kufikia mkataba mpya wa dunia wa mabadiliko ya tabia nchi

https://p.dw.com/p/1AFOl
Mkutano wa tabia nchi waanza Poland kwa wiki mbili
Mkutano wa tabia nchi waanza Poland kwa wiki mbiliPicha: Reuters

Juu ya kwamba hakuna maamuzi makubwa yanayotarajiwa kufikiwa katika mkutano huo unaoanza leo mjini Warsaw, unaweza kuwa dokezo kwa fursa za dunia kufikia makubaliano ifikapo mwaka 2015.

"Uharibifu na Hasara" kwa kielelezo hiki mjumbe amelitaja suala ambalo litakuwa na dhima muhimu katika mkutano wa Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Kielelezo hicho kinakusudia uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ambao hauwezi kuzuilika na hata kama kunajengwa maboma makuu ya kuzuwiya maji au majengo yanayoweza kuhimili vimbunga vikali.

Thomas Hirsch afisa wa sera za maendeleo wa Shirika la Misaada la Ujerumani anasema mtu hawezi kukwepa kusema kwamba matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile ukame na vimbunga husababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Wajumbe katika mkutano wa 19 wa tabia nchi
Wajumbe katika mkutano wa 19 wa tabia nchiPicha: Reuters

Anasema pia huwezi kuepusha kuzama kwa visiwa vidogo vya matumbawe na anataja mfano wa visiwa vya Carteret vilioko katika bahari ya Pasifiki ya Kusini.

Visiwa hivyo katika kipindi cha miaka 25 iliopita vilipoteza asilimia 60 ya ardhi yao na baadhi ya visiwa hivyo vimemeguka kati kati. Wakaazi takriban 3,000 wa visiwa hivyo kwa miaka kadhaa wamekuwa wakiitaka serikali kuwapatia makaazi mapya.

Mambo yatakayotoa majadiliano magumu katika mutano

Lakini kupatiwa makaazi mapya kwa watu hao hakufanyiki kwa sababu serikali haijuwi pa kuwapeleka watu hao na jinsi ya kugharimia zoezi hilo. Katika mkutano wa Poland unaoanza leo hadi tarehe 22 Novemba suala hilo pia litakuwepo kwenye agenda kwa sababu mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi uliofanyika Doha nchini Qatar hapo mwaka jana uliwapa wajumbe wa kushughulikia mkutano huu wa kilele wa Warsaw majukumu ya kuanzisha utaratibu wa kimataifa kushughulikia suala la hasara na uharibifu.

Lakini vipi hasa utaratibu huo utaanzishwa litakuwa suala la majadiliano magumu huko Warsaw. Nchi zenye maendeleo ya viwanda hususan Marekani kwa vyo vyote vile zinataka kuepuka kuingia kwenye makubaliano ya kimataifa ya kisheria ambayo yataziwajibisha nchi kulipa fidia kwa uharibifu fidia ambayo haifanyiwi mahesabu kwa kuzingatia mitizamo ya wakati huu.

Naibu waziri mkuu wa zamani wa Qatar Abdullah Bin Hamad Al-Attiyah, katika mkiutano wa Warsaw
Naibu waziri mkuu wa zamani wa Qatar Abdullah Bin Hamad Al-Attiyah, katika mkiutano wa WarsawPicha: Reuters

Kwa wawakilishi wa mataifa ya visiwa vidogo vilioko hatarini kutoweka halikadhalika kwa nchi maskini na zile zenye maendeleo duni duniani ahadi madhubuti kwa nchi hizo ni muhimu. Mjumbe wa Ujerumani kutoka Wizara ya Mazingira Nicole Wilke anayafafanisha mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya mabadiliko ya tabia nchi na mbio ndefu za marathon.

Hata hivyo ni suala la kutiliwa mashaka iwapo onyo la wanasayansi linatosha kuyapigisha hatua mazungumzo ya Warsaw. Sio Ujerumani ambayo bado haina serikali kufuatia uchaguzi wa mwezi wa Septemba na wala Umoja wa Ulaya zitaweza kuwa na msukumo mkubwa katika mazungumzo hayo.

Mwandsihi: Andrea Rönsberg /Mohamed Dahman

Mhariri: Amina Abubakar