1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa OPEC wamalizika Saudia

Mohamed Dahman19 Novemba 2007

Ilikuwa ni mapinduzi daima mwishoni mwa juma hili nchini Saudi Arabia wakati nchi hiyo ilipokuwa mwenyeji wa Mkutano wa Viongozi wa OPEC Jumuiya ya Nchi Zenye Kuzalisha Mafuta kwa wingi duniani ambapo sauti za viongozi wawili wa nchi wanachama mashuhuri kwa mtindo wao wa kupinga mataifa ya magahribi zilihanikiza kwenye nchi hiyo yenye udhibiti mkali na yenye kuunga mkono mataifa ya magharibi.

https://p.dw.com/p/CIma
Rais Hugo Chavez wa Venezuela achemsha Saudi Arabia kwa kauli za yadumu mapinduzi.
Rais Hugo Chavez wa Venezuela achemsha Saudi Arabia kwa kauli za yadumu mapinduzi.Picha: AP

Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran na Rais Hugo Chavez wa Venezuela waliingiza nuru ya hamasa ya kimapinduzi ambayo haikuwahi kushuhudiwa kabla nchini Saudi Arabia tokea mtetezi wa haki za nchi zinazoendelea wa Misri Rais Gamal Abdel Nasser kuitembelea nchi hiyo hapo mwaka 1956.

Chavez ambaye amejitangaza kuwa mtetezi wa maskini amejigamba juu ya uwezo wa jumuiya hiyo kuhakikisha bei za juu za mafuta kwa maslahi ya nchi zinazoendelea ili kufidia kwa kile kinachoonekana kuwa dhuluma ya mataifa yalioendelea kwa dunia nzima.

Mfalme Abdullah ambaye nchi yake inalipia kuungwa mkono na Marekani kwa kuregeza msumari wa bei za mafuta ambazo zinaweza kuutingisha uchumi wa mataifa ya kitajiri yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani alibakia kimya bila ya tabasamu kama vile walivyo viongozi wengine wa Kiarabu wa mataifa ya Ghuba.

Katika mahala kulikozaliwa Uislamu Chavez alionyesha ishara ya msalaba na kumtaja Yesu Kristo kama kichocheo katika mapambano ya kupinga ukoloni dhidi ya mataifa ya magharibi ambapo anaona OPEC ni mtetezi wa mstari wa mbele.

Ameuambia mkutano huo njia pekee kuelekea amani kama alivyosema Yesu Kristo ni haki na kwamba wote waliokuweko hapo walikuwa wamejishighulisha kwenye mapambano ya nchi za kimaskini,watu waliotumbukizwa kwenya ukoloni,waliovamiwa na kukandamizwa kwa karne chungu nzima.

Chavez anasema wanafuatilia hali nchini Iraq,wameshuhudia vitisho dhidi ya nchi mwanachama ya Iran na anafikiri OPEC lazima iwe imara zaidi na kudai kuheshimiwa kwa haki ya nchi zao kujitawala iwapo nchi zenye maendeleo makubwa ya viwanda zinataka kuendelea kuhakikishiwa kupatiwa mafuta.

Saudi Arabia imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani tokea miaka ya 1950 ikiwa kama hakikisho la usambazaji wa mafuta ghafi kwenye masoko ya dunia kwa kutumia hadhi yake ya kuwa na usemi mkubwa kwenye jumuiya ya OPEC.

Ikiwa watawala wa Saudia wanatafautiana na Chavez hali kama hiyo pia inajiri na Iran.

Saudi Arabia inashirikiana mashaka na Marekani kwamba mpango wa nuklea wa Iran ni njia ya kujipatia silaha za nuklea ili kubadili uwiano wa mataifa yenye nguvu katika eneo hilo kutoka serikali zinazounga mkono mataifa ya magharibi kama vile Israel, Misri na Saudi Arabia.

Rais Ahmedinejad wa Iran ameuambia mkutano wa waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano wa viongozi wa OPEC kwamba vitisho vya hatua ya kijeshi vya Marekani juu ya mipango ya nuklea ya nchi hiyo ni sehemu ya mipango ya nchi hiyo kunyakuwa rasilmali za eneo hilo.

Chavez ameonya kwamba iwapo Marekani itashambulia Iran bei ya mafuta inaweza kuongezeka maradufu na kufikia dola 200 lakini Ahmedinejad amesema Iran haitotumia mafuta kama silaha.

Mkutano huo wa viongozi wa OPEC umemalizika kwa tafauti kubwa ya kisiasa juu ya hatua ya kuchukuwa dhidi ya kuanguka kwa thamani ya dola sarafu ya Marekani.