1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa ´´masikini`` Mali

Nijimbere, Gregoire7 Julai 2008

Wakati viongozi kutoka kundi la nchi 8 tajiri zaidi kiviwanda duniani ama G8 wameuanza mkutano wao nchini Japan, kuna mkutano mwingine unaofanyika nchini Mali kuukosoa mkutano huo wa G8.

https://p.dw.com/p/EXna
Sanamu za eneo la karibu na Bamako Mali

Waandalizi wa mkutano huo unaofaniyka mjini Katigoubou, umbali wa kilomita kama 100 hivi mashariki mwa mji mkuu wa Mali Bamako, waliutaja ´´mkutano wa masikini´´ wakilinganisha na ule unaofanyika Japan ambao unazijumuisha nchi 8 tajiri zaidi duniani. Wanaohudhuria mkutano huo nchini Mali sio viongozi wa nchi au serikali au wawakilishi wao, bali ni wawakilishi wa mashirika ya kujitegemea NGO´s mashirika ya kutetea haki za binaadamu na mashirika ya kijamii yanaohusika na maswala ya kimaendeleo na ambayo ni wakosoaji wa kundi la nchi hizo tajiri zaidi duniani G8.

Katika hotuba yake ya uzinduzi wa mkutano huo, Bi Barry Aminata Touré mwenyekiti wa shirikisho la mashirika yanayopigania maendeleo na kuondolewa kwa deni la nchi masikini kwa nchi tajiri CAD, alisema kunahitajika sheria sawa duniani kuhakikisha kuwa swala la maendeleo limetiliwa maanani.

Kwa sasa amezidi kusema Barry Aminata Touré sheria haipo na nchi masikini hazina mategemeo makubwa kwa mkutano huo wa nchi tajiri nchini Japan na mikutano mengine kama hiyo:

´´Wao watatilia kipau mbele mabadiliko ya hali ya hewa. Sisi tunafikiria kuwa kiini hasa cha mabadiliko hayo, ni uporaji wa rasili mali zetu. Na katika kujikusanyia rasili mali hizo, wanaharibu mazingira. Ingekuwa vyema wakasikiliza zisemavyo jamii´´.

Waandalizi wa mkutano huo wanauliza kwa nini wawakilishi wa nchi 8 tajiri zaidi wanajifungania ndani ya nyumba na kuamua juu ya dunia nzima bila kuzingatia maslahi ya watu wote kwa jumla? Aliuliza Barry Aminata Touré:

´´Kundi la G8 halijapewa ruhusa na nchi na jamii ili liweze kuamuwa juu yao na kuchukuwa hatua katika nafasi ya serikali zetu. Bora G8 la nchi tajiri ligeuzwe G8 umma yaani kundi la umma´´


Mkutano huo wa nchini Mali utakuwa fursa nyingine ya kuzungumzia malalamiko ya nchi zinazoendelea dhidi ya nchi tajiri ikizingatiwa kuwa ahadi za misaada hazitekelezwi, mazingira yamezidi kuharibiwa na viwanda vya nchi tajiri na madhara makubwa kuziathiri nchi nyingine kuliko nchi hizo zilizoyasababisha matatizo hayo bila kusahau masharti ya mashirika ya kifedha ya kimataifa yanayokwamisha maendeleo.

Maada nyingine kama vile elimu barani Afrika, ushirikiano kwa ajili ya mendeleo na deni la nchi zinazoendelea kwa nchi tajiri, zitajadiliwa pia katika mkutano huo utakaokamilisha shughuli zake jumatano siku ambapo utakamilika pia mkutano huo wa nchi tajiri zaidi G8 wa nchini Japan.