1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Marrakesh wafikia kikomo

18 Novemba 2016

Mkutano wa UN huko Marrakesh, Morocco unafikia kikomo hii leo huku kukiwa na hofu kuwa lengo la kuzuia mabadiliko ya tabia nchi huenda lisiafikiwe iwapo hakutakuwa na uungwaji mkono kutoka Marekani.

https://p.dw.com/p/2SsTp
Marokko COP22 Konferenz in Marrakesh
Picha: DW/L. Osborne

Mkutano wa kwanza wa Umoja wa mataifa kuhusiana na hali ya hewa tangu kuidhinishwa kwa mkataba wa Paris mwaka jana wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ulikuwa na jukumu la kuratibu utaratibu wa utekelezaji.Takriban mataifa 200 yaliohusika katika mkataba huo wa Paris yalitoa wito wa pamoja wa kujitolea kikamilifu kukabiliana na mabadiliko hayo ya tabia nchi. 
Wengi wanahofia kwamba Trump ambaye alitaja mabadiliko hayo ya tabia nchi kuwa uwongo uliobuniwa na China atatekeleza kitisho chake cha kujiondoa katika mkataba huo.

Hasara ya kujiondoa kwa Marekani

Kujiondoa kwa Marekani pia kutasababisha kukosekana kwa mabilioni ya dola za kufadhili mataifa yanayoendelea kutumia kawi salama ama njia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambazo haziwezi kuepukika kwa sasa.

Mkataba huo wa Paris una lengo la kupunguza mabadiliko ya tabia nchi hadi kiwango cha nyuzi joto 2.0 kwa kukabiliana na uchafuzi wa hewa kwa utumiaji wa nishati salama.

Mataifa yanayojumuisha Marekani  yalikuwa yameahidi kukabiliana na uchafuzi wa hewa katika mkataba huo kwa kuhimiza matumizi ya nishati inayoweza kutumika tena. 

Marokko COP22 Konferenz in Marrakesh
Mshiriki katika kongamano la MarrakeshPicha: DW/L. Osborne

Lakini Tump ameahidi kuimarisha matumizi ya mafuta, gesi na mkaa.
Kulingana na wachambuzi, bila kuwepo kwa Marekani katika mkataba huo, itakuwa vigumu kuuafikia.
"Uwezo wa mataifa mengine kuchangia katika kupunguza uchafuzi wa hewa kama ilivyokuwa imejitolea Marekani ama kuziba nakisi ya ufadhili uliokuwa umeahidiwa na Marekani ni mgumu kutimiza," alisema Mohammed Adow wa shirika la msaada la Christian linalofuatilia mashauriano kuhusu hali ya hewa kwa niaba ya mataifa maskini." 

Huku ikisubiriwa kwa rais mteule wa Marekani kutangaza msimamo wake kuhusiana na mabadiliko ya tabia nchi, wengi sasa wanatazama mataifa mengine ulimwenguni kutekeleza mkataba huo wa Paris. 
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wa mataifa na serikali pamoja na mawaziri, kila msemaji alisisitiza kujitolea kwa nchi yake katika kutekeleza mkataba huo. Hapo jana mataifa kama vile Brazil, Afrika Kusini, India na China yalisisitiza kuwa yataendelea na kuimarisha juhudu zao huku yakisisitiza kuwa hakuna kurejea nyuma kwa mataifa yalioendelea na hakuna majaribio ya kujadili upya masuala yalioafikiwa katika mkataba huo wa Paris.

Mwandishi: Tatu Karema/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo