1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kuzuia hatari ya kinyuklia duniani waanza

Abdu Said Mtullya24 Machi 2014

Viongozi wa nchi na wakuu wa serikali kutoka duniani kote, pamoja na wajumbe wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine kadhaa wanakutana mjini The Hague ili kujadili njia za kuzuia hatari ya kinyuklia duniani.

https://p.dw.com/p/1BUo5
Rais wa Marekani Barrack Obama
Rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Reuters

Viongozi kutoka nchi 53 wanaanza mkutano wao wa kilele katika mji wa Uholanzi wa The Hague kujadili njia za kuzuia hatari ya silaha za nyuklia kutumiwa na magaidi.

Kwenye mkutano wao siku mbili viongozi hao pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa pia watazungumzia juu ya njia za kupunguza nyenzo za kinyuklia duniani ambazo siyo za kijeshi.

Marais wa Marekani Barack Obama na wa China XI Jingping pia wanahudhuria mkutano huo.

Waziri wa mambo ya nje Urusi, Sergei Lavrov ameshawasili mjini The Hague kwa ajili ya mkutano huo.

Marais hao na viongozi wengine kutoka kote duniani kwenye mkutano wao wa siku mbili wataziangalia njia za kuhakikisha kwamba nyenzo za kinyuklia hazingii katika mikono ya makundi ya kigaidi kama Al-Qaeda.

Rais wa China Xi Jinping, na mwanamfalme wa uholanzi Willem Alexander
Rais wa China Xi Jinping, na mwanamfalme wa uholanzi Willem AlexanderPicha: picture-alliance/AP

Mkutano huo wa kilele unaofanyika kila baada ya miaka mwili unafanyika kwa mara ya tatu tokea uanzishwe kutokana na wazo la Rais Obama mnamo mwaka wa 2009.

Juhudi za kimataifa zinasonga mbele ingawa mpaka sasa magaidi hawajafanya mashambulio kwa kutumia silaha za nyuklia. Wataalamu wanaamini kwamba hatari ya silaha za nyuklia kutumiwa na magaidi siyo jambo la kubuni.

Msingi wa Usalama wa nyuklia kujadiliwa katika mkutano

Magaidi wa Chechen pia walijaribu kuzitumia silaha za sumu mjini Moscow. Hata hivyo pana wasi wasi huenda mkutano huo juu ya usalama wa kinyuklia ukagubikwa na mgogoro wa Ukraine. Lakini Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte amesema mgogoro wa Ukraine hautagongana na ajenda ya mkutano huo.

Pia ameeleza kwamba mkutano kama huo juu ya masuala ya usalama unaweza kuwa fursa nzuri ya kuyajadili masuala mengine vile vile kama mgogoro wa Ukraine.

Waziri mkuu wa Uholanzi ameeleza kuwa viongozi wa dunia kwenye mkutano wao wa siku mbili wanatarajiwa kuweka msingi wa usalama wa nyuklia, yaani mpango thabiti wa kuhakikisha kwamba nyenzo za kinyuklia haziingii katika mikono ya magaidi.

Wataalamu wa silaha za nyuklia
Wataalamu wa silaha za nyukliaPicha: picture alliance/ROPI

Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni zipo tani 1390 za madini ya uran duniani, yaliyorutubishwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo pia zipo tani 490 za madini ya Plutonium duniani. Na kati ya hizo kiasi ya tani 260 zinatumika kwa madhumuni ya amani, kama vile kwa ajili ya tiba.

Mwandishi: Over,Veronica.

Tafsiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Gakuba, Daniel