Gut, aber nicht gut genug
12 Desemba 2011Kwa mara nyengine tena imedhihirika katika mkutano huu wa Durban kwamba walimwengu hawana moyo wa kisiasa kuweza kukabiliana ipasavyo na mabadiliko ya tabia nchi. Mataifa mengi yanataka kuchangia kidogo tu. Marekani, Canada, Rashia, India na China-tukiyataja mataifa hayo matano tu.
Kizazi kipya kitakapotafakari yaliyofikiwa wakati wa mikutano kama hii ya kimataifa, basi nionavyo mie jibu lao litakuwa kali kupita kiasi. Kwasababu tunatambua kile tukifanyacho.
Kwanza upande wa kisayansi: watafiti wa hali ya hewa kwa miaka sasa wamekuwa wakionya: ikiwa moshi unaotoka viwandani hautapunguzwa haraka na kwa kiwango kikubwa, basi balaa la kuzidi ujoto katika sayari yetu halitaepukika.
Pili: kwa upande wa kiufundi, tuna kila kitu kinachohitajika kuweza kutengeneza nishati isiyochafua hali ya hewa. Nishati inayotokana na nguvu za upepo, inapatikana tayari kwa bei hafifu sawa na nishati inayotokana na mafuta, na nguvu za jua. Upepo na juwa vinapatikana pomoni katika dunia yetu kuweza kukidhi sehemu kubwa ya mahitaji ya nishati inayopatikana kutokana na makaa mawe, mafuta na gesi.
Tatu: Ni kwa upande wa kiuchumi mwanauchumi wa Uengereza Nicholas Stern ameonya katika ripoti yake, miaka chungu nzima iliyopita kwamba madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yatatugharimu fedha nyingi zaidi ikiwa hatutawajibika kuanzia sasa.
Lakini wanasiasa hawafanyi chochote: Sababu ni nyingi tuu. kwanza hali hiyo inatokana na ushawishi wa mashirika makubwa makubwa ya nishati, mfano ya mafuta na makaa mawe yanayohofia kuondoka patupu, mfumo wa sasa utakapofanyiwa marekebisho. Na sababu nyengine inatokana na ukosefu wa shinikizo la umma.Yadhihirika kana kwamba watu wanahisi mabadiliko ya tabia nchi si jambo linalotuhusu hivyo, kwa hivyo hakuna haja ya watu kuingiwa na wasiwasi.
Kwa watu wengi wa nchi masikini, kwa maneno mengine,wale ambao hawahusiki hata kidogo na kuchafuliwa hali ya hewa, kuzidi hali ya ujoto duniani inamaanisha kupungua mavuno, ukame, njaa na mafuriko. Kwa nchi hizo mabadiliko ya tabia nchi si suala la nyuzi joto,bali suala la kufa kupona.
Uamuzi wa Durban ni wa maana. La maana pia ni kuona itifaki ya Kyoto inarefushwa kwa kipindi kipya kinachozitaka nchi zote ziwajibike. La maana pia ni kuona kwamba majadiliano yamesaidia kufikiwa makubaliano timamu yanayozijumuisha pia nchi zinazoinukia na ambayo yataanza kufanya kazi kuanzia mwaka 2018.
Lakini hayo hayatoshi- kwasababu mkutano huu wa Durban peke yake hautoshi kuzuwia mabadiliko ya tabia nchi. Ndio maana majadiliano ziada yanahitajika.
Mwandishi:Beck Johannes/Hamidou Oummilkheir.
Mhariri: Miraji Othman