1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya

19 Desemba 2013

Viongozi wa Umoja wa Ulaya Wanajiandaa Kuidhinisha Makubaliano ya Kihistoria ya Kuundwa Umoja wa Benki kati ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Sarafu

https://p.dw.com/p/1AcUO
Kansela Angela Merkel (kushoto),rais Francois Hollande na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Alain Jocard/AFP/Getty Images

Umoja wa Ulaya umepiga hatua muhimu na ya kihistoria kuelekea muungano mpana zaidi,masaa machache kabla ya mkutano wa kilele unaoanza hii leo,kwa kufikia makubaliano kuhusu muungano wa benki uliolenga kuepusha lisirejee tena balaa la mgogoro wa fedha katika nchi za kanda ya Euro.

Makubaliano hayo yanayofungua mlango wa kukabidhiwa umoja wa Ulaya,mamlaka ya kitaifa,hatua ya aina pekee kuwahi kupitishwa tangu umoja wa sarafu ulipoanzishwa,yataidhinishwa wakati wa mkutano wa viongozi unaoanza hii leo,akishiriki pia kansela Angela Merkel,ambae ndio kwanza ameapishwa upya kwa mhula mwengine wa miaka minne madarakani.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuyapa nguvu madai ya kansela Angela Merkel mbele ya viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya, kujenga Umoja wa Ulaya wenyewe nguvu zaidi,chini ya mhimili madhubuti wa uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa.

Akichaguliwa kwa mhula wa tatu kua kiongozi wa nchi yenye uchumi madhubuti kabisa barani Ulaya,kansela Angela Merkel amesisitiza pia msimamo wake wa kuendelezwa mageuzi yasiyopendwa ili kudhamini utulivu wa bajeti ya nchi za Umoja wa Ulaya.

Umoja wa benki wafikiwa

Masaa machache kabla ya mkutano wa kilele kuanza,wanachama 28 wa umoja wa Ulaya wamejadiliana kwa kina kuhusu mkataba wa kuundwa bodi ya polisi,kuzifunga benki zinazokabwa na matatizo,kubuni fuko la kugharimia mipango hiyo na yote hayo bila ya kutumia fedha za fuko la walipa kodi.

Wolfgang Schäuble Treffen der EU Finanzminister in Brüssel 18.12.2013
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: DW/B. Riegert

Nchi zote 17,zinazotumia sarafu ya pamoja ya Euro zitalazimika kufuata mfumo uliowekwa huku mataifa mengine yakiwachia uwezekano wa kujiunga baadae.

Waziri wa fedha wa Ufaransa Pierre Muscovici ameyataja makubaliano yaliyofikiwa kuwa ni ya kihistoria.Mwenzake wa Ujerumani Wolfgang Schäuble anasema:

"Umoja wa Benki ni hatua muhimu katika juhudi za maana za kuituliza sarafu ya pamoja na kutuliza masoko ya hisa ili yatambue kwamba sarafu ya Ulaya,licha ya muundo wake, ni madhubuti na ndio maana umoja wa benki unahitajika."

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia masuala ya masoko ya hisa ameyataja makubaliano yaliyofikiwa kuwa ni "mageuzi ya kimapinduzi katika mfumo wa benki barani Ulaya kwa namna ambayo walipa kodi hawatolazimika kubebeshwa jukumu la kuchangia benki zitakapokumbwa na migogoro.

Uhusiano madhubuti kati ya Ufaransa na Ujerumani

Kansela Angela Merkel alishadidia lengo la kuuimarisha umoja wa ulaya alipokutana na rais wa Ufaransa Francois Hollande mjini Paris jana.Amesema tunanukuu"Kwa ushirikiano pamoja na Ufaransa tunataka kuifanya Ulaya liwe bara lenye nguvu ulimwenguni."

Merkel Regierungserklärung 18.12.2013
Kansela Angela MerkelPicha: picture alliance/AP Photo

Mbali na masuala ya kiuchumi,mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utazungumzia pia mzozo wa Ukraine ,Syria na hali katika jamhuri ya Afrika kati.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman