1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels

Hamidou, Oumilkher16 Oktoba 2008

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanafikiria uwezekano wa kubuni "serikali ya kiuchumi"

https://p.dw.com/p/FbPK
Rais Sarkozy wa Ufaransa na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya BarrosoPicha: AP



Mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya,rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amesema mwishoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja huo mjini Brussels hii leo,atashauri mkakati wa ushirikiano wa kiuchumi kwa nchi 27 za umoja wa ulaya kabla ya mwaka huu kumalizika.



Rais Sarkozy anasema kuna umuhimu wa kuendelezwa mpango wa kuufumbua  mzozo wa fedha uliofikiwa mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Paris.


Akizungumza na waandishi habari mwishoni mwa mkutano wa kilele wa umoja wa Ulaya  hii leo mjini Brussels,rais Sarkozy amesema anapanga kutangaza mkakati huo hadi ifikapo january mosi mwakani.


Rais Nicolas Sarkozy ameendelea kusema:



"Ulaya nzima,inaunga mkono hatua zilizopitishwa jumapili iliyopita na viongozi wa nchi zinazotumia sarafu ya Yuro mjini Paris.Kutokana na mzozo huu usiokua na mfano,nchi 27 za Umoja wa Ulaya zina jibu moja tuu;jibu la nguvu lenye muongozo madhubuti."


Kiongozi huyo wa Ufaransa amezungumzia uwezekano wa kuibuka serikali ya kiuchumi ya Ulaya,kufuatia mkutano wa kilele wa jumapili iliyopita.


"Suala nililowauliza viongozi wa taifa na serikali,mie kama mwenyekiti wa Umoja wa ulaya ni kwamba:ikiwa tumefanikiwa kuupatia jibu la pamoja mzozo wa fedha barani Ulaya,si ingekua bora kuupatia pia jibu la pamoja mzozo wa kiuchumi barani Ulaya" ameshadidia rais Nicolas Sarkozy,huku akijiuliza tunanukuu:


"Kulikua na hali ya mkorogano,sasa tunafuata njia bora,kwa hivyo tuendelee kuifuata.Suala ni jee tuendelee na ushirikiano katika sekta ya kiuchumi sawa na tunavyoshirikiana katika mzozo wa fedha?Mwisho wa kumnukuu mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya aliyesema jibu la nchi yake ni "ndio".



Rais Nicolas Sarkozy amekumbusha kwamba mataifa wanachama wa Umoja wa ulaya yameitaka halmashauri kuu ya Umoja hzuo ibuni mkakati wa namna ya kusaidia ukuaji wa kiuchumi na kuhimiza kubuniwa nafasi za kazi.Kipa umbele ni sekta ya kiviwaanda.


Kwa mara nyengine tena mwenyekiti huyo wa zamu wa Umoja wa Ulaya ametetea haja ya kuitishwa mkutano wa kimataifa kudurusu mfumo wa fedha wa dunia,kabla ya kumalizika mhula wa rais Georg W. Bush wa Marekani.


Sawa na kansela Angela Merkel wa Ujerumani,na waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown,na yeye pia amezungumzia umuhimu wa kufafanuliwa jukumu la shirika la fedha la kimataifa IMF.