1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa nchi za kiarabu mjini Doha

Oumilkher Hamidou30 Machi 2009

Viongozi wa kiarabu wanapanga kuzungumzia mpango wa amani wa mashariki ya kati

https://p.dw.com/p/HMf7
Katibu mkuu wa jumuia ya nchi za kiarabu Amr Moussa (kushoto) akipokeklewa uwanja wa ndege wa Doha na waaziri wa mambo ya nchi za nje wa Qatar (kulia)Picha: AP


Viongozi wa kiarabu wameanza mkutano wao wa mwaka hii leo mjini Doha nchini Qatar,akihudhuria pia rais wa Sudan Omar el Bashir licha ya amri ya korti ya kimataifa ya uhalifu inayotaka akamatwe.


Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon atahudhuria pia mkutano huo wa kilele licha ya kuwepo rais Omar al Bashir.


Lakini mkutano huo uliolengwa kuleta suluhu miongoni mwa mataifa ya kiarabu unasusiwa na rais Hosni Mubarak wa Misri,pamoja pia na viongozi  wa Maroko,Algeria,Iraq na Oman.


Hii ni ziara ya nne ya rais wa Sudan nchi za nje tangu korti ya kimataifa ya uhalifu ilipotangaza amri ya kukamatwa al Bashir March 4 mwaka huu,kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadam.


Muendesha mashtaka mkuu wa korti hiyo,Moreno-Ocampo anaisihi jumuia ya nchi za kiarabu na kusema:


"Nnahisi jumuia ya nchi za kiarabu inabidi ianzishe majadiliano ya kuupatia ufumbuzi mzozo wa Darfour.Ikiwa kuna atakaeweza kufanya hivyo basi  ni jumuia ya nchi za kiarabu.Kwa hivyo nnamini  viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu wana jukumu kubwa la kuona namna ya kuufumbua mzozo huo hivi sasa na namna ya kumtanabahisha Bashir abadilishe uamuzi wake."


Jumuia hiyo ya kiarabu yenye wanachama 22 inazozana katika suala la hujuma za hivi karibuni za kijeshi za Israel huko Gaza.


Kuna makundi mawili.Moja linaongozwa na Syria na Qatar na kuwaunga mkono Hamas na kundi la pili linaongozwa na Saud Arabia na Misri ambazo zinaelemea zaidi upande wa rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas na chama chake cha Fatah.


Juhudi za mfalme Abndallah wa Saud Arabia,aliyechangia kuitisha mkutano mdogo wa kilele huko Kuweit january mwaka huu na baadae mjini Riyadh march 11 iliyopita,zilizusha matumaini mema,lakini matumaini hayo yamefifia baada ya rais Mubarak kuususia mkutano huu wa kilele wa Doha.


Mkutano wa kilele wa nchi za kiarabu unatazamiwa pia kuzungumzia mustakbal wa mpango wa amani wa nchi za kiarabu ulioshauriwa mwaka 2002 na ambao unaahidi kurejesha uhusiano wa kawaida pamoja na Israel ikiwa kwa upande wake itarejesha ardhi za waarabu inazozikalia tangu mwaka 1967.


Mwishoni mwa mkutano wao hapo kesho mchana,viongozi wa nchi za kiarabu wamepanga kukutana na viongozi wa mataifa 12 ya kusini mwa bara la Amerika,kwa mkutano wa pili wa kilele uliolengwa kufungua njia ya ushirikiano kati ya kambi hizo mbili.