1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Riyadh-Saud Arabia unamalizika hii leo

Oummilkheir29 Machi 2007

Israel yasema mpango wa amani hauwezi kukubalika kama ulivyo hivi sasa

https://p.dw.com/p/CHHE
Mfalme Abdallah wa Saud Arabia katika mkutano wa viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini Riyadh
Mfalme Abdallah wa Saud Arabia katika mkutano wa viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu mjini RiyadhPicha: AP

Mkutano wa kilele wa viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu umeingia katika siku yake ya pili na ya mwisho hii leo mjini Riyadh nchini Saud Arabia.Jana viongozi hao waliunga mkono kwa sauti moja mpango wa amani pamoja na Israel mpango ambao Israel inasema haiwezi kuutambua kama ulivyo.

Viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu wanaokutana mjini Riyadh Saud Arabia wameamua kwa sauti moja kutia njiani mpango wa amani pamoja na Israel ulioshauriwa kwa mara ya kwanza mwaka 2002.Viongozi hao wamewatolea mwito serikali na wananchi wote wa Israel waukubali mpango huo.

Mpango huo ulioidhinishwa kwa mara ya kwanza wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi hao Beyrouth ,miaka mitano iliyopita unazungumzia juu ya uhusiano wa kawaida pamoja na Israel,ikiwa kwa upande wake Israel itayahama maeneo yote ya waarabu inayoyakalia tangu mwaka 1967,ikiwa ni pamoja na milima ya Golan ya Syria , eneo la kusini mwa Libnan , kuundwa dola ya Palastina na kurejea nyumbani wakimbizi wa Palastina.

Naibu waziri mkuu wa Israel,Shimon Peres amesema hii leo “hawawezi kuukubali kama ulivyo mpango huo”.Akizungumza kupitia Radio ya taifa mshindi huyo wa zawadi ya amani ya Nobel amesema tunanukuu”Njia pekee ya kumaliza tofauti zilizoko ni mazungumzo.Tukikubali mpango huu kama ulivyo,hakutakua na maana ya kujadiliana”Mwisho wa kumnukuu Shimon Peres.

Israel inapendelea baadhi ya vifungu vya mpango huo vifanyiwe marekebisho na hasa kuhusiana na haki ya kurejea nyumbani wakimbizi wa Palastina na mipaka ya dola la siku za mbele la Palastina.

Viongozi wa Israel wanahisi mpango huo wa amani unaweza kutumiwa kama msingi wa majadiliano ikiwa utafafanua kwamba wakimbizi wa kipalastina warejee katika maeneo yanayodhibitiwa na Palastina na sio nchini Israel

Mjini Jerusalem kwenyewe mamia ya waisrael wanaopinga kukaliwa ardhi za wapalastina walikusanyika jana mbele ya ofisi ya waziri mkuu Ehud Olmert mjini Jerusalem kumtaka aunge mkono mpango wa amani wa jumuia ya nchi za kiarabu.

Viongozi wa jumuia ya nchi za kiarabu wamezungumzia pia mzozo wa Libnan na Sudan.

Kuhusu mzozo wa Sudan mfalme Abdallah wa Saud Arabia amesema.

“Uzembe wa jumuia ya nchi za kiarabu ndio sababu ya kuhitajika vikosi kutoka nje.Yote haya yanatokea huku sisi tukijiacha kando,hatuna tunalolifanya kuwasaidia ndugu zetu.”

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon ,alizungumza na rais Omar el Bashir wa Sudan,pembezoni mwa mkutano wa kilele wa mjini Riyadh hapo jana.Duru za kuaminika zinasema mazungumzo yao yamehusiana na mzozo wa Darfour na jinsi ya kutia njiani makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya mjini Khartoum na Umoja wa mataifa.

”Rais Bachir hajatoa jibu lolote la maana mpaka sasa” amesema muakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa ulaya Javier Solana anaehudhuria pia mkutano huo wa kilele mjini Riyadh.

Wakati huo huo duru za kuaminika kutoka mji mkuu wa Suudia zinasema mkutano kuhusu jimbo hilo la magharibi ya Sudan,ulikua ufanyike jana usiku kati ya mfalme Abdallah wa Saud Arabia,rais Omar El Bashir wa Sudan na mkuu wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Alpha Omar Konare.