1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Kilele wa G20 waanza China

5 Septemba 2016

Mkutano wa kilele wa siku mbili wa kundi la G20 umefunguliwa nchini China Jumapiliv (04.09.2016) kwa wito kwa chombo hicho kuwa timu ya vitendo badala ya kuwa mahala pa kupiga porojo.

https://p.dw.com/p/1JvYl
Picha: picture-alliance/dpa/B.v. Jutrczenka

Akifunguwa mkutano huo katika mji wa Hangzhou Rais Xi Jinping wa China amesema anataraji huko Hangzhou wanaweza kushughulikia dalili za matatizo halikadhalika sababu kuu za matatizo ya uchumi wa dunia ....."G20 inapaswa ibadili mtizamo wake na kuweka umuhimu sawa kwa sera za muda mfupi na sera za muda mrefu."

China ni mwenyeji wa viongozi 20 wa kundi hilo la nchi zenye maendeleo makubwa ya kiuchumi duniani na zile zenye kuinukia kiuchumi katika mji mashuhuri wa kihistoria wa Hangzhou ulioko mashariki mwa China kuanzia Jumapili (04.09.2016) hadi Jumatatu ambapo usalama umeimarishwa kwa kuwekwa kwa vikwazo barabarani.

Rasi Xi alisalimiana kwa kupeana mikono na wageni waliokuwa wakiingia mmoja baada ya mwengine katika kituo cha Maonyesho ya Kibiashara cha Kimataifa cha Hangzhou kunakofanyika mkutano huo miongoni mwao Rais Barack Obama wa Marekani, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Vladimir Putin wa Urusi, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini.

Dhima ya China

Tukio hilo linaonyesha dhima ya China katika jukwaa la dunia wakati baadhi ya viongozi wakitarajiwa kuishinikiza China kutii kanuni za kimataifa za biashara na uzaslihaji wake wa kupindukia wa chuma.

Rais Xi Jinping wa China wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kilele wa G20.
Rais Xi Jinping wa China wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kilele wa G20.Picha: Reuters/A. Song

Katika hotuba yake ya ufunguzi Rais Xi amesema kundi hilo la G20 halipaswi kuchukuwa hatua mpya za kuhami masoko na badala yake ichukuwe hatua madhubuti za kuchochea ukuaji wa uchumi duniani.

Obama na XI walikutana Jumamosi jioni ambapo nchi zote mbili zilitangaza kujiunga rasmi na makubaliano ya Paris ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Wakati wa mazungumzo yao yaliochukuwa muda mrefu Xi aliihimiza Marekani kutimiza dhima yenye tija katika kudumisha amani na utulivu katika eneo la Bahari ya China Kusini.China inadai kumiliki takriban eneo lote hilo ambalo pia linagombaniwa na Vietnam, Taiwan,Ufilipino,Malaysia na Brunei.

Nafasi ya vyombo vya habari yaleta tafrani

Mkutano wa Xi na Obama ulitiwa kiwingu na mzozo kuhusu suala la vyombo vya habari kuuangazia mkutano huo ambapo hapo Jumapili Rais Obama alikiri kwamba kulikuwepo na mvutano kuhusiana na sisitizo la Marekani la kujumuishwa kwa vyombo vya habari wakati wa Mkutano huo wa kilele wa kundi la mataifa 20 ambapo amesema hatoomba radhi kwa kuvitetea vyombo vya habari.

Akizungumza katika mkutano huo Obama amesema "tunafikiri ni muhimu kwamba vyombo vya habari vinapatiwa nafasi ya kuelewa kazi tunayoifanya ili wawe na uwezo wa kujibu maswali. Hatuyaachi nyuma maadili yetu wakati tunapofanya safari hizi."

Mzozo huo ulianza mara baada ya kutuwa kwa ndege ya Air Force One katika mji wa Hangzhou hapo Jumamosi ambapo kundi la waandishi wa Kimarekani lililokuwa likiandamana na Rais Obama lilipozuiliwa wakati rais alipokuwa akiteremka kwenye ndege ambapo afisa wa China aliwapigia makelele wafanyakazi wa Ikulu ya Marekani kuwaondowa kabisa waandishi wa habari katika eneo hilo.

Rais Barack Obama wa Marekani akizungumza na waandishi wa habari mjini Hangzhou.
Rais Barack Obama wa Marekani akizungumza na waandishi wa habari mjini Hangzhou.Picha: Reuters/J. Ernst

Wakati afisa wa Ikulu aliposema hilo lilikuwa ni suala linamhusu rais wa Marekani na kwamba hiyo ilikuwa ni ndege ya Marekani kwa hiyo waandishi hao wataendelea kubakia katika eneo hilo afisa huyo wa China alijibu kwa ukali kwamba "Hii ni nchi yetu".

Afisa huyo pia alipapurana na Mshauri wa Usalama wa Taifa Susan Rice na Naibu Mshauri wa Usalama wa Taifa Ben Rhodes wakati walipokuwa wakijaribu kutembea karibu na Rais Obama.Kuhusiana na kisa hicho Rice alisema baadae "Wamefanya mambo ambayo hawakuyategemea."

Mvutano huo uliendelea tena hapo Jumapili wakati sehemu ya mkururo wa vyombo vya habari uliokuwa ukimsindikiza Obama ulipozuiliwa kukaribia eneo la mapokezi la mkutano huo wa kilele wa G20.

Mbali na suala la ukuaji wa uchumi mkutano huo unatowa fursa kwa viongozi kujadili masuala mbali mbali muhimu duniani.

Mwandishi : Mohamed Dahman /dpa/AP

Mhariri :Saumu Mwasimba