1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa kilele mjini Damascus

Hamidou, Oumilkher4 Septemba 2008

Rais Nicholas Sarkozy azungumzia mashariki ya kati pamoja na rais Bachar Al Assaad wa Syria,Amir wa Qatar Sheiklh Hamad Bin Khalifa Al-Thani na waziri mkuu wa Uturuki Tayeb Erdogan

https://p.dw.com/p/FBBu
Rais Bachar Al Assad akiamkiana na rais Sarkozy baada ya kuwasili DamascusPicha: AP



Mwenyekiti wa Umoja wa ulaya,rais Nicholas Sarkozy wa Ufaransa amemaliza ziara ya siku mbili mjini Damascus Syria kwa kuhudhuria mkutano wa pande nne uliowaleta pamoja viongozi wa Ufaransa,Syria,Qatar na Uturuki.Mkutano huo umelenga kufufua mazungumzo ya amani kati ya Syria na Israel.


Mada mbili kuu zimehodhi mkutano huo wa kilele wa pande nne :mazungumzo ya kichini chini kati ya Israel na Syria chini ya upatanishi wa Uturuki na uhusiano kati ya Syria na Libnan.Iran pia ilidhukuriwa mazungumzoni.


Rais Nicholas Sarkozy ambae pia ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa ulaya alizungumza kwa muda wa saa nzima pamoja na rais mwenzake wa Syria Bachar el Assad,mwenyekiti wa jumuia ya nchi za kiarabu,Amir wa Qatar Cheikh Hamad ben Khalifa Al Thani ambae ni mwenyekiti wa baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba aliyechangia sana katika kupatiwa ufumbuzi mzozo wa Libnan na waziri mkuu wa uturuki Tayeeb Erdogan ambae nchi yake inaemndesha juhudi za kichini chini za kufufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na Syria.


Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Ufaransa kuitembelea Syria baada ya kupita zaidi ya miaka mitano.Rais Sarkozy anasema :


"Tunataka hatua baada ya hatua kujenga uhusiano ambao tunataka uwe wa kuaminiana na kugeuza ukurasa wa hitilafu za maoni."


Kwa maoni ya rais Nicholas Sarkozy,si makosa kuishughulikia mizozo yote ya eneo hilo kwa wakati mmoja.Anasema tunamnukuu"Nnahisi ni jambo la busara kufanya hivyo kwasababu mizozo yote ya eneo la mashariki ya kati ina ingiliana na inafungamana.Kuuacha kando mzozo huu au ule,ni kosa "amesema rais huyo wa Ufaransa ambae ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya.


Rais Nicholas Sarkozy ameishukuru Uturuki kwa mchango wake katika kurahisisha mazungumzo kati ya Israel na Syria.


"Waturuki wamefanya kazi kubwa itakayopelekea kuanza mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Syria na Ulaya nzima inashukuria."


Kwa upande wake rais Bacher El Assad amesisiza wanasubiri uchaguzi wa bunge nchini Israel ili kuamua mustakbal wa mazungumzo hayo.Amesema wanataka kupata uhakika kama waziri mkuu mpya wa Israel atafuata nyayo za Ehud Olmert linapohusika suala la kuihama Israel milima ya Golan.


Rais Bacher El Assad ameongeza kusema wanasubiri pia kuona nani atashinda uchaguzi wa rais nchini Marekani.


Duru nne za mazungumzo ya siri zimeshafanyika hadi sasa kati ya Syria na Israel na ya tano iliyokua iitishwe September sabaa ijayo imeakhirishwa baada ya kujiuzuklu mkuu wa tume ya Israel katika mazungumzo hayo Yoram TURBOWITZ.