Mkutano wa jumuia ya OSCE. | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.12.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa jumuia ya OSCE.

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, leo umeingia siku yake ya pili na ya mwisho, kwa kufanya majadiliano ya kina kuweza kufikia muafaka wa kuweza kujiimarisha na kuepukana na mizozo.

default

Rais wa Kazakhstan Nursultan Nazarbayev(kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Viongozi wanaohudhuria mkutano huo, ambao unafanyika katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana wamekiri kwamba  uwezo wa jumuia hiyo ya Usalama na Ushirikiano barani Ulaya kuweza kutekeleza malengo yake ya kuzuia mizozo barani Ulaya na katika nchi za uliokuwa muungano wa zamani wa Kisovieti umefifia katika siku za hivi karibuni.

Baada ya saa kadhaa za mazungumzo ya faragha, wanadiplomasia wanaohudhuria mkutano huo wamesema kwamba makubaliano kamili yamechelewa kufikiwa kutokana na kutoafikiana kwa baadhi ya masuala yanayozihusu nchi zilizokuwa katika muungano wa zamani wa kisovieti, ikiwemo suala la Georgia pamoja na mvutano kati Armenia na Azerbaijan.

Katika mkutano huo, rais wa Armenia Serzh Sarkisian na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev, walitoa hotuba zilizozua mivutano kati yao, ambapo kila mmoja alikuwa akimlaumu mwenziye kwa kuhujumu mazungumzo ya kutafuta suluhu kuhusuana na mzozo wa Nagorny Karabakh.

Jumuia hiyo ya OSCE Yenye wanachama 56, inafanya kazi kwa kutegemea makubaliano ya pamoja, kwa maana ya kuwa taifa moja linaweza kuvuruga makubaliano na pendekezo la hatua, ambayo wanadiplomasia wanatarajia itaweza kubadilisha mustakabali wa mchango wa jumuia hiyo ya OSCE.

Aidha katika mkutano huo wito pia ulitolewa wa kufanyiwa marekebisho ya kina jumuia hiyo iliyoundwa wakati wa vita baridi, ili kuhimiza majadiliano kati ya pande mbili na ambayo imedhorota tangu vita baridi vilipomalizika.

Mkutano kama huo wa jumuia hiyo ya Usalama na ushirikiano barani Ulaya umepangwa kufanyika tena mwaka ujao  nchini Lithuania.

Wakati huohuo akizungumza leo pembezoni mwa mkutano huo wa Jumuia ya Usalama na Ushirikiano barani ulaya unaofanyika katika mji wa Astana Kazakhstan, Waziri Mkuu wa Italia Silvio Berlusconi amekanusha madai yaliyokuwemo katika nyaraka za kidiplomasia zilizovuja za Marekani kwamba  

uhusiano wake wa karibu na Urusi ulikuwa ni wa maslahi binafsi.

Waziri mkuu wa Italy alikuwa akijibu swali kuhusiana na nyaraka zilizotumwa kwenye internet na mtandao wa Wikileaks ambazo nyaraka hizo zilisema kwamba Wamarekani wanaamini kuwa Berlusconi ananufaika kutokana na makubaliano mengi ya nishati katika ya Urusi na Italy.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,afp)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 02.12.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QOIY
 • Tarehe 02.12.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/QOIY

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com