1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa hali ya hewa wafunguliwa Copenhagen

Oumilkher Hamidou7 Desemba 2009

Wajumbe 15.000 wahudhuria mkutano wa wiki mbili kuinusuru dunia yetu na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa

https://p.dw.com/p/Kri8
Moshi wa viwanda vya mafuta unachafua hali ya hewaPicha: AP

Mkutano wa kimataifa kuhusu kupunguzwa moshi unaotoka viwandani,unaoangaliwa kua chanzo cha kuzidi hali ya ujoto duniani,umefunguliwa leo mjini Copenhagen nchini Danemark,pakiwepo matumaini mema ya kufikiwa maridhiano kufuatia ahadi zilizotolewa mnamo siku za hivi karibuni.

Katika wakati ambapo majadiliano yalionekana kukwama miaka miwili ya nyuma,matumaini ya kufikiwa makubaliano yamechomoza kufuatia uamuzi wa viongozi chungu nzima wa taifa na serikali kushiriki katika mkutano huo pamoja pia na ahadi zilizotolewa na jumla ya mataifa yanayochafua zaidi mazingira,ikiwa ni pamoja na China,Marekani,Urusi na India,kupunguza viwango vya moshi unaotoka viwandani.

Majadiliano yatakayodumu karibu wiki mbili,yatamalizika kwa mkutano wa kilele utakaowaleta pamoja viongozi 105 wa taifa na serikali-rais Barack Obama wa Marekani atashiriki mkutanoni December 18,-mkutano utakaokua na jukumu la kumaliza tofauti za vya mwisho mwisho zilizopo kati ya nchi masikini na nchi tajiri kuhusu namna ya kugawana mzigo wa kupunguza moshi wa viwandani.

Viongozi wa taifa na serikali hawakushiriki katika mkutano uliopita wa mawaziri wa mazingira,mnamo mwaka 1997-uliopelekea kutiwa saini mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu hali ya hewa mashuhuri kwa jina la "itifaki ya Kyoto."

Dänemark Klimakonferenz Kopenhagen Bella Center Pressekonferenz
Yvo de Boer (wa pili kutoka kushoto) katika mkutano na waandishi habari mjini CopenhagenPicha: AP

"Copenhagen ndio nguzo ya jibu la kimataifa kwa mabadiliko ya hali ya hewa" amesema hayo mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa la hali ya hewa,Yvo de Boer na kuendelea:

" Tukizungumzia juu ya gharama za muda mfupi ,basi kwa mwaka,tangu mwaka 2010,2011 na 2012,tutabidi kukusanya kila mwaka daka bilioni 10 ili kudhamini gharama za kupunguza moshi wa viwandani na kugharimia mipango ya kuinusuru hali ya hewa.Tunajua kwamba kwa mtazamo wa muda mrefu,fedha zaidi zitahitajika.Tukitaka kuzungumzia kuhusu miradi ya baada ya mwaka 2020 na 2030,hapo tutazungumzia juu ya mamia kwa mabilioni ya dala."

Mkutano wa Copenhagen ni mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mikutano ya kimataifa kuhusu hali ya hewa.Wajumbe 15 elfu kutoka nchi 195 watajaribu kuiepushia dunia yetu madhara yanayosababishwa na kuchafuka hali ya hewa,ikiwa ni pamoja na ukame,kuenea jangwa,kupanda usawa wa bahari na kadhalika.

Afrika kusini imetangaza hata kabla ya kutuma ujumbe wake mkutanoni mjini Copenhagen,inapanga kupunguza moshi wa viwandani kwa chini ya asili mia 34 hadi ifikapo mwaka 2020 ikiwa nchi tajiri zitaisaidia kifedha na kiufundi kulifikia lengo hilo.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/ afp/dpa

Mhariri:Abdul-Rahman