Mkutano wa G8 wamalizika
20 Mei 2012Kwenye tamko lao la pamoja viongozi hao wamesema kuwa wamekubaliana kwa pamoja kuchukua hatua zinazohitajika kuinua na kuuimarisha uchumi wa nchi zao na kuudhibiti mtikisiko wa kifedha huku wakitambua kuwa hatua hizo hazitafanana kwa kila nchi.
Ujumbe huo wa jumla ambao ulisomwa na mwenyeji wa Mkutano huo wa siku mbili Rais wa Marekani Barack Obama, kwa kiasi fulani umerandana na mapendekezo yake kwamba mzozo wa uchumi wa kanda hiyo ambao kwa sasa unatishia hatma ya umoja huo wa nchi 17 unaweza kuuathiri pia uchumi wa nchi yake na kuvuruga fursa za kushinda uchaguzi wa Novemba.
Kanda ya euro yazidi kukabiliwa na matatizo
Kutokana na hali tata ya kisiasa na kiuchumi inayoikabili Ugiriki, kupungua kwa thamani ya fedha na mzozo wa madeni unaozidi kuchomoza Italia na Uhispania ambapo hisa zimekuwa zikishuka kwa kiwango kikubwa kila leo kundi hilo limekubaliana kuyatazama masuala hayo kwa utulivu zaidi na kurekebisha hali hiyo.
Kwenye hitimisho la mjadala wao wa kiuchumi, viongozi hao wametoa wito wa kuongezwa juhudi za kuutatua mzozo huo huku wakiunga mkono msimamo wa Ujerumani wa kubana matuimizi kwa nchi husika, kujiimarisha kiuchumi na kuongeza fursa za ajira.
Kuhusu uwezekano wa Ugiriki kujiuondoa kwenye kanda ya sarafu ya Euro, viongozi hao kwa pamoja wamesema kuwa nia yao ni kuiona nchi hiyo ikendelea kubaki kwenye umoja huo lakini pia wamesema wanaheshimu maamuzi ya nchi hiyo.
Wajadili pia Afghanistan na mashariki ya kati
Ni jambo lisilo la kawaida kwa mataiafa hayo tajiri kukaa na kuizunguumzia nchi ndogo kama hiyo, hofu ya kuwa hali ya mtafaruku wa kisiasa nchini humo unaweza kusababisha nchi hiyo kujiondoa kwenye kanda ya sarafu ya Euro kunawatia mashaka wakihofia kuporomoka kwa masoko na uchumi wa dunia kwa ujumla.
Wapiga kura nchiuni Ugiriki mwezi huu waliwaadhibu viongozi wa nchi hiyo wanaoungamkono mpango wa kubana matumizi kwa kutumia kura zao kwenye uchaguzi, na kisababisha yafanyaike marudio June 17 ambapo hadi sasa bado wingu la wasiwasi bado limetanda.
Mkutano huo pia ulijadili masuala mengine yakiwemo ya kisiasa ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa kimataifa ikiwemo hali ilivyo nchini Afghanistan na Mashariki ya Kati.
Kundi la G8 linaundwa na nchi za Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Canada, Italia, Uingereza, Urusi na Japan na mkutano wa safari hii umefanyika huko Camp David mjini Maryland nchini Marekani chini ya uenyeji wa Rais wa nchi hiyo Barack Obama.
Mwandishi: Stumai George
Mhariri: Sekione Kitojo