1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G8 wajishughulisha zaidi na mataifa ya Kiarabu

27 Mei 2011

Katika siku ya kwanza ya mkutano wa kundi la mataifa ya G8 nchini Ufaransa, uasi uliotokea katika mataifa ya kiarabu umewashughulisha zaidi viongozi wa kundi hilo, wakiahidi kuzisaidia nchi hizo.

https://p.dw.com/p/11Otf
Viongozi wa mataifa ya G8 wanaonekana wakati wa majadiliano katika meza ya duara mjini Deauville nchini Ufaransa ambako mkutano wa mataifa hayo unafanyika.Picha: dapd

Katika siku ya kwanza ya mkutano wa kundi la mataifa ya G8 nchini ufaransa, uasi uliotokea katika mataifa ya kiarabu umewashughulisha zaidi viongozi wa kundi hilo.Rais Nicolas Sarkozy ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo amesema katika ufunguzi wa mkutano huo katika mji wa Deauville kuwa ana matumaini wakati huu mpya wa msingi utasambaa katika eneo lote la Afrika kaskazini. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi msaada zaidi kwa mataifa yanayoinukia katika demokrasia katika eneo la mataifa ya kiarabu.

G8 Gipfel Frankreich Mai 2011
Rais Sarkozy akimkaribisha kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika mkutano wa G8Picha: dapd

Kundi la viongozi wa mataifa hayo manane yenye utajiri mkubwa wa viwanda duniani walitarajiwa kuidhinisha msaada wa mabilioni ya dola kwa mataifa ya Kiarabu ambayo yako katika harakati za kutekeleza demokrasia katika mpango ambao una lengo la kuimarisha mabadiliko yanayotokea katika maeneo ya Afrika ya kaskazini na mashariki ya kati.

Viongozi hao walitarajiwa kukamilisha mkutano wao wa siku mbili kaskazini mwa Ufaransa kwa kuanzisha ushirika na eneo hilo ambao unahusisha misaada pamoja na fedha za maendeleo kwa maendeleo ya kidemokrasi katika mataifa ambayo yamewaondoa viongozi madikteta.

Tunisia na Misri , ambazo mawaziri wao wakuu watakutana na viongozi wa kundi hilo la G8, la mataifa saba ya magharibi pamoja na Urusi leo Ijumaa , wanakabiliwa na mbinyo mkubwa wa kiuchumi kufuatia vuguvugu la mapinduzi ambalo limesababisha kuangushwa kutoka madarakani kwa viongozi wa muda mrefu ambao ni madikteta.

Katika ripoti kwa viongozi wa kundi la G8 shirika la fedha la kimataifa IMF limesema siku ya Alhamis kuwa mahitaji ya fedha katika mataifa yanayoagiza mafuta katika mashariki ya kati na Afrika kaskazini yatafikia kiasi cha dola bilioni 160 katika muda wa miaka mitatu ijayo.

Eneo hilo linahitaji kujitayarisha na mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchumi wao, Masood Ahmed , anayehusika na eneo la mashariki ya kati na Afrika ya kaskazini katika shirika la fedha la kimataifa IMF, amewaambia waandishi habari pembezoni mwa mkutano wa G8 mjini Deauville.

Hali hii itawezekana iwapo jumuiya ya kimataifa ikiwa ni pamoja na mataifa ya G8 itaingia katika ushirikiano wa kimkakati na nchi hizi, ambapo vivutio vinahusishwa na agenda ya mambo ya kijamii.

IMF inasema kuwa inaweza kutoa kiasi cha dola bilioni 35 kusaidia kuimarisha uchumi wa nchi hizi lakini sehemu kubwa ya fedha zitahitajika kutoka katika jumuiya ya kimataifa.

Benki kuu ya dunia siku ya Jumanne wiki hii imetangaza msaada mpya wa dola bilioni 6 kwa Tunisia na Misri, nchi ambazo uasi wa wananchi umetia hamasa kwa watu wa Yemen, Jordan, Morocco na Syria, na kumlazimisha kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi kupambana ili kubaki madarakani.

Fedha hizo ni pamoja na msaada katika bajeti pamoja na fedha zitakazosaidia kuinua sekta ya binafsi pamoja na kutia nguvu uwekezaji mpya.

G8 Gipfel Frankreich Mai 2011 Obama Medvedev
Rais Barack Obama wa Marekani na rais wa Urusi Dmitry Medvedev wakitembea pamoja wakati wakiwasili kwa ajili ya mkutano wa G8Picha: AP

Duru za kidiplomasia zinasema kuwa mkutano huu pia utaunga mkono kurefushwa kwa muda wa benki ya Ulaya ya ujenzi mpya na maendeleo katika Afrika ya kaskazini na mashariki ya kati.

Benki hiyo iliyoundwa baada ya vita baridi kusaidia mataifa ya zamani ya Ulaya mashariki kuwa na uchumi unaovutia masoko, inatoa kiasi cha euro bilioni 9 kila mwaka kwa miradi katika mataifa ya Croatia katika Ulaya ya kati hadi China.

Wakati huo huo Marekani , Ufaransa na Canada zimeongeza miito yao kumtaka rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh kujiuzulu, baada ya mapigano ya usiku kucha kuuwa darzeni kadha za watu.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre