1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G8 wafikia ukingoni

Admin.WagnerD18 Juni 2013

Viongozi wa nchi nane zilizoendelea kiviwanda duniani G8 wanajadili kuhusu jinsi ya kuzuia kutekwa nyara kwa wafanyakazi wa kigeni katika nchi za Afrika na kuyadhibiti makampuni yanayohama hama ili yalipe kodi.

https://p.dw.com/p/18rZ9
Picha: Jewel SamadAFP/Getty Images

Viongozi hao tangu jana wamekuwa wakijaribu kutafuta kuafikia kauli ya pamoja kuhusu mzozo wa zaidi ya miaka miwili wa Syria huku Rais wa urusi Vladimir Putin anayeunga mkono utawala wa Rais Bashar al Assad akikataa kubadili msimamo wake kuhusu suala hilo.

Viongozi wa mataifa saba akiwemo Rais Barrack Obama wameonyesha kuwaunga mkono waasi wanotaka kumng'oa madarakani Assad.Nchi hizo ni pamoja na mwenyeji ji wa mkutano huo wa G8 Uingereza, Japan,Ufaransa,Ujerumani,Italy, Canada,Urusi na Marekani.

Viongozi hao wanamshinikiza Putin kujiunga nao kuhusu Syria au akabiliwe na hatari ya kutengwa. Obama na Putin walijaribu kuficha tofauti zao kuhusiana na mvutano huo lakini wamekubaliana kuendelea na mipango ya kuandaa mkutano wa Geneva kimataifa wa kutafuta amani Syria.

Rais wa Urusi Vladimir Putin,Cameron na Obama
Rais wa Urusi Vladimir Putin,Cameron na ObamaPicha: Reuters

Utekaji nyara Afrika wazungumziwa

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anatafuta uungwaji mkono kuhusu suala la kulipa fidia kwa watekaji nyara kama hatua ya kukabiliana na tatizo hilo kufuatia utekaji nyara wa wafanyakazi wa kigeni katika kiwanda cha gesi nchini Algeria na kuuawa kwao wakiwemo pia raia 40 wa Algeria.

Utekaji nyara wa wafanyakazi wa kigeni umeongezeka hasa katika mataifa ya magharibi mwa Afrika hususan Nigeria ambako sekta yake ya mafuta imetawaliwa na kampuni za magharibi na wasimamizi wa kigeni.

Wakati uo huo,Rais wa benki ya maendeleo ya Afrika Donald Kaberuka ameusifu mkutano huo wa G8 kwa kuangazia suala la kuboresha sekta ya mali asili ya bara la Afrika kupitia uwazi katika ulipaji wa kodi.

Viongozi wa G8 katika meza ya mazungumzo
Viongozi wa G8 katika meza ya mazungumzoPicha: Reuters

Afrika ina uwezo wa kujiboresha

Kebaruka ameihimiza jamii ya kimataifa kuendeleza uwazi,kupunguza ukwepaji kodi na kuhakikisha kandarasi za kuhusu mali asili zinaafikiwa kwa njia ya haki bila kupunja upande mmoja wa mapatano na kuongeza haya yakiafikiwa, basi mataifa ya Afrika yataweza kugharamia ukarabati wa miundo mbinu na kupanua biashara miongoni mwao mambo ambayo mpaka sasa yanategemea ufadhili wa nchi za kigeni.

Cameron pia amewaalika viongozi wa Libya na wa Umoja wa Afrika kujiunga katika meza ya mazungumzo leo.Mkutano huo unaokamilika leo unashuhudia misururu ya mikutano ya viongozi wanaohudhuria na wanahabari kabla ya kuondoka Uingereza huku Rais Obama akiendeelea na ziara yake ya bara ulaya kwa kutarajiwa kuwasili Ujerumani leo jioni.

Mwandishi: Caro Robi/ap/afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman