1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba kumalizika leo

7 Desemba 2010

Nchi za kiarabu katika eneo la Ghuba zinayatazama kwa jicho la wasiwasi mazungumzo ya Geneva kati ya nchi zenye nguvu na jirani yake Iran kuhusiana na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo. Nchi za Ghuba zinahisi zimetengwa

https://p.dw.com/p/QRhV
Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahayan (kulia) na viongozi wa baraza la ushirikiano wa nchi za GhubaPicha: AP

Katika mkutano wa kilele wa baraza la ushirikiano wa nchi za Ghuba unaomaliza hii leo (07.12.2010) waziri wa mambo ya nje wa Emarati amezikosoa wazi nchi za magharibi kwa kuwatenga majirani wa Iran kushiriki mkutano unajadili suala la Nuklia la nchi hiyo.

Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahayan amehoji ni kwanini nchi hizo za Magharibi zinahisi suala hilo la Iran linawahusu wao pekee? Suluhisho lolote kuhusiana na suala hilo la mradi wa Nuklia wa Iran linabidi kutoka nchi za eneo hilo na kutambuliwa kwamba nchi wanachama wa baraza la ushirikiano katika eneo la Ghuba zinajukumu katika mazungumzo hayo .

Iran inafanya mazungumzo ya siku mbili huko Geneva yanayomalizika leo pamoja na nchi wanachama wa kudumu ndani ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa,ambazo ni Uingereza,China,Ufaransa,Urussi na Marekani pamoja na Ujerumani. Mazungumzo hayo ya Geneva yanafanyika sambamba na mkutano wa nchi za Ghuba wa GCC unaoandaliwa kila mwishoni mwa mwaka. Katika mkutano wa nchi za Ghuba kikubwa kinachojadiliwa huko Abu Dhabi ni hofu ya nchi hizo iliyowekwa wazi katika nyaraka kadhaa za kidiplomasia za Marekani nyaraka ambazo zilichapishwa katika mtandao wa Wiki Leaks.

Mhadhiri na mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika chuo kikuu cha Emarati Ibtisam Ketbi amesema kwamba bila shaka kutafikiwa makubaliano kati ya Wairani na Wamarekani lakini makubaliano hayo yatakuwa kwa gharama ya nchi hizo za Ghuba,kwa maneno mengine ni makubaliano yatakayoziweka pabaya nchi hizo za Ghuba majirani wa Iran.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema Nchi za Magharibi zinaweza kukubali mpango wa Iran ikiwa zitapewa uhakika na Iran kwamba utakuwa mpango wa amani japokuwa hili ni jambo lisilopendelewa na Israeli ambao wanaushirikiana wa karibu na Marekani. Hata hivyo baadhi ya maafisa wa katika mkutano huo wa Abu Dhabi wanahisi kwamba hakuna maafikiano yoyote yatakayoweza kupatikana kati ya Iran na nchi za Magharibi.

Senatorin Hillary Clinton, 20.01.2007
Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani, Hillary ClintonPicha: AP

Wiki iliyopita waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton alisema kwamba Tehran inaweza kutengeneza madini ya Uranium kwa ajili ya matumizi ya kiraia ikiwa itathibitisha kufanya hivyo kwa njia ya uwazi.Matamshi hayo yalipongezwa sana na Iran.

Aidha katika mkutano huo uliomalizika jumapili huko Manama waziri wa Iran aliwatoa hofu majirani wake wa nchi za kiarabu na kusema nchi yake haiwezi hata siku moja kuzishambulia nchi za kiislamu.Lakini katika taarifa zilizochapishwa na mtandao wa Wiki Leaks imebainika kwamba nchi zote za kiarabu katika Ghuba zimejawa na hofu kuhusu mpango huo wa siri wa Iran wa kutengeneza silaha za Kinuklia licha ya kwamba Iran imeshasema mara zote kwamba haina nia ya kutengeneza silaha hizo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: AbdulRahman