1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika waujadili usalama wa kikanda

16 Juni 2015

Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika umekamilika mjini Johannesburg, ijapokuwa ulighubikwa na suala la mahakama nchini humo kutaka kukamatwa kwa Rais wa Sudan Omar al Bashir

https://p.dw.com/p/1FhoU
Gipfel Afrikanische Union AU in Addis Abeba 2015
Picha: picture-alliance/dpa/Gcis/Siyasanga Mbambani

Bashir anatakikana na mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu ya ICC yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi.

Mada kuu ya mkutano huo wa kielele wa 25 wa Umoja wa Afrika mwaka huu ilikuwa ni kulenga kuwawezesha wanawake na maendeleo kuelekea kufikiwa kwa ajenda ya Afrika ifikapo mwaka 2063. Masuala mengine ambayo viongozi wa nchi takriban hamsini za Afrika waliyajadili ni usalama wa kanda na mpango wa muda mrefu wa maendeleo barani humo.

Hata hivyo agizo la mahakama lililotolewa siku ya ufunguzi wa mkutano huo siku ya Jumapili dhidi ya Rais wa Sudan Omar al Bashir ulimulikwa zaidi na kutia ukungu ajenda kuu za mkutano huo.

Omar al-Bashir in Sudan
Rais wa Sudan Omar al-Bashir akiwasili Khartoum kutoka Afrika KusiniPicha: picture-alliance/dpa/M. Ali

Mahakama moja Afrika Kusini ilikuwa imeagiza Rais huyo anayetakikana na mahakama ya ICC kutoruhusiwa kuondoka nchini humo hadi mahakama hiyo itakaposikiliza kesi hiyo na kutoa uamuzi wa iwapo akamatwe na kusalimishwa kwa mahakama ya ICC au la.

Hata hivyo al Bashir aliweza kuondoka nchini humo jana na kurejea nchini mwake alikolalikiwa kwa furaha na wafuasi wake. Alipowasili katika uwanja wa ndege na kutua kutoka ndege iliyokuwa imembeba,Rais huyo alinyoosha bakora yake hewani huku mamia ya raia wake wakimkaribisha kwa kusema Mungu ni mkubwa na mahakama ya ICC imeshindwa.

Mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda amesema amevunjwa moyo na kushindwa kwa Afrika Kusini kumkamata na kumsalimisha kiongozi huyo wa Sudan anayetakikana na mahakama hiyo ya kimataifa kwa mashitaka ya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki yaliyotokea katika jimbo la Darfur, nchini Sudan ambapo takriban watu laki tatu waliuawa na milioni mbili kuachwa bila ya makaazi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema mamlaka ya mahaka ya ICC yanapaswa kuheshimiwa. Marekani pia imeelezea kuvunjwa moyo na kushindwa kwa serikali ya Afrika Kusini kumzuia na kumkamata Al Bashir na badala yake kumruhusu kuondoka nchini humo.

Jaji Dunstan Mlambo wa mahaka ya Pretoria ameishutumu serikali ya Afrika Kusini kwa kukiuka maagizo ya mahakama ambayo ilitoa kibali cha kukamatwa kwa Bashir bila ya kufahamu kuwa tayari ameshaondoka nchini humo.

Smail Chergui
Kamishna wa Umoja wa Afrika kuhusu amani na usalama Smail CherguiPicha: picture-alliance/dpa/M. Reynolds

waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan Ibrahim Ghandour amesema Rais Al Bashir ataendelea kushiriki katika mikutano ya kimataifa kama kawaida na juhudi zozote za kumtatiza kiongozi huyo wa Sudan hazitawateteresha.

Mbali na hayo, viongozi hao wa Afrika wamezindua majadiliano ya mpango wa kuwepo eneo la biashara huru barani Afrika ujulikanao kwa kifupi CFTA. Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema CFTA inalenga kulisogesha mbele bara la Afrika

Aidha viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika waliweza kukubaliana katika kikao cha kuhitimisha mkutano huo wa kilele hapo jana kuwatuma wataalamu wa kijeshi nchini Burundi ambako kuna ghasia zilizochochewa na tangazo la Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuwa atagombea muhula wa tatu madarakani.

Kamishna wa Umoja wa Afrika kuhusu amani na usalama Smail Chergui amewaambia wanahabari kuwa viongozi wa nchi wamekubaliana kutuma wataalamu wa kijeshi kuhakiki shughuli ya kuwakopokonya silaha wapiganaji wa makundi yaliyo na silaha Burundi.

Cherugui amesema kiasi ya watalaamu 50 watatumwa nchini humo kufuatilia kinachojiri na kutoa ushauri kwa polisi iwapo kutakuwa na haja ya kufanya hivyo.

Viongozi wa Afrika wametoa wito kuwe na suluhisho la kisiasa linalokubalika na pande zinazozana kwa kuzileta pande hizo zote kushiriki katika mazungumnzo.

Mwandishi:Caro Robi/afp/reuters
Mhariri: Hamidou Oummilkheir