1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Afghanistan The Hague

31 Machi 2009

Mkono wa suluhu kwa watalibani watakaoachana na itikadi kali.

https://p.dw.com/p/HNhY
Rais Obama na KarzaiPicha: AP

Wajumbe kutoka nchi 90 mbali mbali usoni kabisa waziri wa nje wa Marekani Bibi Hillary Clinton,Katibu mkuu wa UM Banki Moon,Rais Hamid Karzai wa Afghanistan na majirani zake wawili: Iran na Pakistan, wanahudhuria mkutano wa leo tu mjini The Hague,Uholanzi juu ya mustakbala wa Afghanistan.

Wakati mjumbe wa Iran, waziri mdogo wa mambo ya nje, Mehdi Akhounzadeh amejitolea nchi yake kuchangia juhudi za kupambana na madawa ya kulevya mpakani mwake na Afghanistan,amesema nchi yake inapinga kuwapo majeshi ya kigeni nchini Afghanistan.

Wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan waliotayari kuachana na itikadi na siasa zao kali wanapaswa kunyoshewa "mkono wa heshima wa suluhu"-alisema Bibi Hillary Clinton ,waziri wa nje wa Marekani.

Bibi Clinton akihutubia leo mkutano mjini The Hague,Uholanzi uliohudhuriwa pia na majirani wawili wa Afghanistan-Iran na Pakistan-siku chache tu baada ya rais Barack Obama kutangaza mkakati wake mpya kukomesha uasi wa kiasi cha miaka 8 wa wataliban nchini humo.

Kabla ya Bibi Clinton kuzungumza, Rais Hamid Karzai alikaribisha juhudi mpya zinazochukuliwa na Rais Barack Obama wa Marekani, kusaka ufumbuzi wa kimkoa juu ya mgogoro sugu wa nchi yake ya Afghanistan: Alisema,

"Ninakaribisha kuzidi kutambuliwa kuwa bila ya ushirikiano wa kweli wa majirani wa Afghanistan,ushindi wa kuuzika ugaidi hauwezi kupatikana."

Iran,ilimpeleka makamo-waziri wake wa nje m kutanoni mjini The Hage-Mehdi Akhoundzadeh,ilisisitiza tena kupinga kwake wanajeshi wa nchi za kigeni katika ardhi ya jirani yake Afghanistan.Hatahivyo, imeahidi itasaidia katika juhudi za za kupambana na biashara ya magendo ya madawa ya kulevya inayostawi mno nchini Afghanistan.

Bibi Clinton na Bw.Akhoundzadeh hawakupangwa kuwa na mazungumzo marrefu mjini The Hague,lakini hawatazamiwi kuepuka kutoonana .

Akibadili sera za mtangulizi wake rais George Bush, utawala wa rais Obama ,umeinyoshea mkono wa suluhu Iran ,licha ya mvutano wa muda mrefu kati ya Washington na Marekani juu ya mradi wa kinuklia wa Iran.kambi ya magharibi yaituhumu Iran kupanga kuunda silaha za nuklia wakati Iran inadai ni mradi wa nishati tu.

Zaidi ya wanajeshi 70,000 wa Marekani na NATO tayari wako nchini Afghanistan kupambana na watalibani na Al Qaeda ambao wanaeneza ushawishi na itikadi zao kali hadi jirani Pakistan. Tangu kushika madaraja januari 20, mwaka huu rais Obama ameamrisha kuongezwa kwa jumla ya askari 17.000 huko kuzima machafuko kabla ya uchaguzi wa hapo august.kikosi kingine cha askari 4000 kitasaidia kulijenga jeshi la Afghanistan.