1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano kuhusu Mashariki ya Kati Lisbon

Maja Dreyer19 Julai 2007

Kwa mara ya kwanza mwakilishi mpya wa jumuiya ya kimataifa kwa eneo la Mashariki ya Kazi, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, leo hii atakutana na pande nne zinazoshughulikia amani Mashariki ya Kati, yaani Umoja wa Mataifa, Marekani, Urusi na Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/CB2g
Tony Blair anaanza kazi yake mpya
Tony Blair anaanza kazi yake mpyaPicha: AP

Tony Blair anatarajiwa kuzungumzia mipango yake ya kuweko taifa la Kipalestina na jukumu lake katika shughuli hiyo.

Wanaotarajiwa kukutana na Tony Blair leo jioni mjini Lisbon ni waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Bi Condoleezza Rice, mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, mwakilishi wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, pamoja na waziri wa nje wa Urusi, Sergei Lavrov. Mazungumzo kati yao yanatarajiwa kuhusu hatua ya rais Bush wa Marekani juu ya kuzifufua upya juhudi za kusaka amani Mashariki ya Kazi akipendekeza kufanywe mkutano wa kimataifa mwezi wa Septemba ili kuyaanzisha tena mazungumzo juu ya mzozo huu.

Vile vile, pande hizo nne zinatarajiwa kuzungumzia jukumu la mpatanishi mpya Blair baada ya ripoti kuchapishwa zinazosema kwamba Wapalestina wanataka jukumu lake Blair liwe kubwa zaidi na kumtaka kuzungumza pia na kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Hamas. Marekani lakini inapinga mazungumzo haya, ikisisitiza kuwa Hamas ni kundi la kigaidi.

Msemaji wa serikali ya Marekani, Sean McCormack, kabla ya mkutano, alisema mkutano huu wa leo huenda hautakuwa na matokeo kamili, lakini ni fursa nzuri kwa pande nne husika kukaa pamoja na kutathmini yale yaliyotokea katika wiki kadhaa zilizopita pamoja na kuangalia mbele.

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, ambaye baada ya kujiuzulu mwishoni mwa mwezi wa June, aliukubali wadhifa huu kama mwakilishi maalum kwa Mashariki ya Kati. Alipoulizwa ikiwa ana matumaini kufika mbali katika kutafuta suluhisho kwa mzozo huu kuliko alivyoweza kama waziri mkuu, Blair alisema: “Faida ambazo rais wa zamani Clinton alizonishauri zinatokana na kwamba unaweza kujihusisha na suala moja tu. Kama waziri mkuu lazima kushughulikie masuala mengi tofauti.”

Faida nyingine kwa waziri mkuu huyu wa zamani ni kuwa tayari anazijua pande zote husika na namna mashirika ya kimataifa yanavyofanya kazi. Hata hivyo, kuteuliwa kwake na rais Bush wa Marekani kumepingwa na makundi ya nchi za Kiarabu kutokana na Blair kuiunga mkono Marekani katika vita vya Iraq na kuipendelea Israel katika vita na Lebanon. Kundi la Fatah la Kipalestina limepokea vizuri kuteuliwa Tony Blair lakini katika barua kwa pande nne zinazoshughulia amani ya Mashariki ya Kati, Fatah imedai Blair pia ashughulikie masharti yaliyowekewa Israel, kama vile kusimamisha ujenzi wa ukuta na makazi ya Wayahudi.

Tony Blair anatarajiwa kuitembelea Israel na maeneo ya Wapalestina wiki ijayo.