Mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na China | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na China

Umoja wa Ulaya unailalamikia China kuhusu sarafu yake ya Yuan

default

Waziri Mkuu wa China asema kuwa nchi yake itaacha soko kuwa na usemi zaidi.

Serikali ya China imefanya mazungumzo na maafisa kutoka Umoja wa Ulaya.Mazungumzo hayo yamehusu sarafu ya China ambayo inaonekana inatishia hali ya Uchumi wa nchi hizo.

Waziri mkuu wa China, Wen Jiabao,amesema leo kuwa nchi yake itaacha soko kuwa na usemi zaidi katika kuchangia kuweka kiwango cha sarafu yake ya Yen.Waziri mkuu amesema hayo baada ya kukutana kwa mazungumzo na vigogo kutoka Ulaya kuhusu mkwaruzano katika masuala ya kibiashara pamoja na ya sarafu.

Maofisa wa Umoja wa Ulaya wamevunjwa moyo na jinsi thamani ya sarafu China –Yuan- inavoshuka dhidi ya sarafu ya Ulaya-Euro -kinyume na utaratibu halisi.Hali hii imezilazimisha nchi za Ulaya kuchukua tahadhari kutokana na kutokuweko na uwiano sawa kati ya Yuan na Euro.

Waziri mkuu wa China ameuambia mkutano wa kibiashara kati ya China na Ulaya kuwa, nchi yake itaendelea, hatua kwa hatua, kuleta uwiano unaofaa, ili kutoa mwanya kwa soko kuwa na usemi zaidi katika masuala ya kuweka kiwango cha ubadilishanaji sarafu.

Matamshi ya Waziri mkuu Wen, yanatilia mkazo kauli ya ya rais wa Benki kuu ya Ulaya,Jean Claude Trichet,alisema kuwa huenda China inachukua mwelekeo wa kuimarisha sarafu yake ya Yuan.

Akizungumza na waandishi habari mjini Beijing, Trichet amesema kuwa wameambiwa kuwa hali hiyo itapigwa darubini.

Kinara wa Benki kuu ya Ulaya ni miongoni mwa vigogo kadhaa kutoka Umoja wa Ulaya ambao wamekwenda China kufanya majadilano mbali mbali na utawala wa huko kuhusu mada tofauti,muhimu zikiwa sera ya sarafu ya China na kile ambacho umoja wa Ulaya unachokiona kama kulegeza kama katika vita dhidi ya bidhaa bandia.

Umoja wa Ulaya umekuwa umejitokeza na hatua kali dhidi ya China katika masuala ya sarafu na biashara,baada ya kuamini kuwa kubembeleza kwao hakujazaa matunda yaliyotarajiwa na tena kwa haraka.

Benki kuu ya Ulaya na benki kuu ya China, zimekubaliana kuunda kamati itakayokuwa na jukumu la kuchunguza masuala ya sarafu,ambayo yamejitokeza kama chanzo kikuu kilichosababisha kutoelewana.

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo kati ya serikali ya China na vigogo wa Umoja wa Ulaya,mwanachama mpya wa kamati kuu ya chama cha kikomunisti,Li Keqiang, amesifu kuimarishwa kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya China na umoja wa Ulaya.

Li Keqiang anatazamiwa kuwa makamu wa waziri mkuu wa China hapo mwakani.

Licha ya sauti ya maridhiano kutoka kwa Li, ishara zote katika kipindi cha siku chache zilizopita,zilionyesha msimamo tofauti kuhusu,sio tu kasi ya mageuzi lakini pia na mwelekeo wa uchumi wa China.

Kamishna wa biashara wa umoja wa Ulaya,Peter Mandeson,nae ameongeza lawama zake dhidi ya China kwa kujikokota kutekeleza haraka matatizo ya usalama wa chakula na bidhaa kutoka China.

 • Tarehe 28.11.2007
 • Mwandishi Siraj Kalyango
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CUFF
 • Tarehe 28.11.2007
 • Mwandishi Siraj Kalyango
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CUFF

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com