1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjuwe Tokyo Sexwale

Sekione Kitojo25 Februari 2016

Tokyo Sexwale anasema anataka kupambana na ubaguzi wa rangi katika Shirikisho la Soka Duniania (FIFA) kwani tangu kuasisiwa kwake mwaka 1904, Waafrika walikuwa wanasota ubaoni.

https://p.dw.com/p/1I2PI
Tokyo Sexwale
Tokyo SexwalePicha: picture-alliance/AP Photo/V. R. Caivano

Mwanaharakati huyo wa zamani aliyepambana dhidi ya ubaguzi wa rangi wakati akitangaza kuwania nafasi hiyo. Waafrika wamesubiri kwa muda wa miaka 111, na sasa kuna haja ya kuondoa ukoloni katika mpira wa miguu.

Kwa muda mrefu sana shirikisho la FIFA limeongozwa na Wazungu. Sexwale ametumikia kifungo cha miaka 13 katika gereza la kisiwa cha Robben, na baada ya kuachiwa mwaka 1990 alikuwa shujaa mkubwa na mwanasiasa maarufu nchini Afrika kusini.

Sexwale mwenye umri wa miaka 62 jina lake halisi ni Mosima Gabriel Sexwale. Jina lake la utani la Tokyo alilipata baadaye kutokana na kupendelea sana mchezo wa karate.

Sexwale ni mgombea pekee kutoka bara la Afrika katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania kuwa rais wa FIFA. Katika mpango wake wa kampeni ya uchaguzi mfanyabiashara huyo tajiri anazungumzia pamoja na mambo mengine , utawala bora wa fedha, uwazi na uwajibikaji.

Kwa haraka chama cha kandanda nchini Afrika kusini SAFA kiliidhinisha nia yake ya kugombea Februari 5 mwaka 2015 , lakini chama hicho hakikuendelea kumuunga mkono zaidi.

Sexwale hajafurahishwa na hatua ya shirikisho la kandanda nchini Afrika kusini kutomuunga mkono. Pia hakujali wakati shirikisho la kandanda barani Afrika CAF, lilipomuunga mkono mgombea mwenzake kutoka Bahrain Sheikh Salman bin Ibrahim Khalifa.

Kwa mujibu wa taarifa za magazeti ya Afrika kusini, vyama vya kandanda barani Afrika havijafurahishwa na utendaji wa Sexwale, na kwamba mipango yake haijakamilika na haitoshelezi maslahi ya kitaifa nchini mwake.

Ukosefu wa uzoefu

Mwandishi wa habari za michezo Mxolisi Ncube amesema katika mahojiano na DW, kwamba Sexwale anakosa uzoefu. "Hajawahi kuongoza klabu ya mpira na hatajafanyakazi na shirikisho la kandanda nchini Afrika kusini, mbali ya kufanyakazi katika kamati ya matangazo kwa ajili ya kombe la dunia mwaka 2010. Haiwakilishi Afrika, badala yake anataka kurukia medani ya kimataifa."

Wagombea urais wa FIFA.
Wagombea urais wa FIFA.

Sexwale hata hivyo hasumbuliwi na hilo na anaendelea kuwamo katika kinyang'anyiro hicho cha uongozi. Anafahamu nini maana ya kushindwa. Akiwa waziri mkuu wa jimbo muhimu nchini Afrika kusini katika miaka ya 1990 alipata tathmini finyu sana. Mwaka 2008 alitaka kuwa mgombea wa kiti cha urais katika chama tawala cha ANC na akashindwa, na akashindwa na mgombea mwenzake ambaye ni maarufu zaidi Jacob Zuma.

Akiwa waziri wa nyumba chini ya utawala wa Zuma hajafanya vya kutosha na miaka miwili baadaye alishindwa tena katika nia yake ya kuwa makamu wa rais wa chama cha ANC.

Hata hivyo Tokyo Sexwale amefanikiwa zaidi akiwa mfanyabiashara. Hivi sasa ni mmoja kati ya watu matajiri sana nchini Afrika kusini.

Mwandishi: Morgenrath, Birgit /ZR/Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef